Mwanzo 16:1-6
Mwanzo 16:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Sarai, mkewe Abramu, alikuwa bado hajamzalia mumewe mtoto. Lakini alikuwa na mjakazi aliyeitwa Hagari, kutoka Misri. Basi, Sarai akamwambia Abramu, “Unajua kuwa Mwenyezi-Mungu hajanijalia kupata watoto. Mchukue Hagari mjakazi wangu; huenda nikapata watoto kwake.” Abramu akakubali shauri la Sarai. Kisha, Sarai akampa Abramu Hagari, mjakazi wake ambaye alikuwa Mmisri, awe mke wake. Haya yalitokea baada ya Abramu kukaa katika nchi ya Kanaani kwa muda wa miaka kumi. Abramu akamchukua Hagari, naye Hagari akapata mimba. Lakini mara tu alipoona amepata mimba, Hagari akaanza kumdharau bimkubwa wake. Sarai akamwambia Abramu, “Wewe utawajibika kwa ubaya ninaotendewa. Mimi nilikupa mjakazi wangu, lakini alipopata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake! Mwenyezi-Mungu na ahukumu kati yako na mimi!” Lakini Abramu akamwambia Sarai, “Mjakazi wako yuko chini ya mamlaka yako; mfanyie upendavyo.” Basi, Sarai akamtesa Hagari mpaka akatoroka.
Mwanzo 16:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, kwa kuwa BWANA amenifunga tumbo nisizae, sasa mwingilie mjakazi wangu, labda nitapata uzao kutoka kwake. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Kwa hiyo, baada ya Abramu kukaa miaka kumi katika nchi ya Kanaani, Sarai mkewe Abramu alimtwaa Hajiri Mmisri, mjakazi wake, akampa Abramu mumewe, kama mke. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bimkubwa alikuwa duni machoni pake. Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe. Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mikononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake.
Mwanzo 16:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake. Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe. Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake.
Mwanzo 16:1-6 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Basi Sarai, mkewe Abramu, alikuwa hajamzalia watoto. Lakini alikuwa na mjakazi Mmisri jina lake Hajiri. Hivyo Sarai akamwambia Abramu, “Mwenyezi Mungu amenizuilia kupata watoto. Basi nenda ukutane kimwili na mjakazi wangu; huenda nitaweza kupata watoto kupitia kwake.” Abramu akakubaliana na lile Sarai alilosema. Hivyo baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani miaka kumi, Sarai akamchukua mjakazi wake Mmisri aliyeitwa Hajiri, na kumpa mumewe awe mke wake. Abramu akakutana kimwili na Hajiri, naye akapata mimba. Hajiri alipojua kuwa ana mimba, akaanza kumdharau Sarai. Ndipo Sarai akamwambia Abramu, “Unawajibika na mateso ninayoyapata. Nilimweka mtumishi wangu mkononi mwako. Sasa kwa vile anajua kwamba ana mimba, ananidharau mimi. Mwenyezi Mungu na aamue kati yako na mimi!” Abramu akamwambia, “Haya, mtumishi wako yuko mkononi mwako. Mtendee lolote utakalo!” Ndipo Sarai akamtesa Hajiri, naye akamtoroka.