Mwanzo 12:9-20
Mwanzo 12:9-20 BHN
Kisha Abramu akaendelea kusafiri kuelekea upande wa Negebu. Wakati huo, njaa ilitokea nchini. Njaa hiyo ilikuwa kali, hivyo Abramu akalazimika kwenda Misri kukaa huko kwa muda. Alipokaribia Misri, Abramu alimwambia Sarai mkewe, “Najua kuwa wewe ni mwanamke mzuri na wa kuvutia. Wamisri watakapokuona watasema, ‘Huyu ni mkewe,’ kisha wataniua lakini wewe watakuacha hai. Basi, waambie kuwa wewe ni dada yangu ili mambo yaniendee vema, niachwe niishi kwa ajili yako.” Basi, Abramu alipowasili nchini Misri, wenyeji wa huko walimwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana. Maofisa wa Farao walipomwona Sarai, wakamsifia kwa Farao. Basi, Sarai akapelekwa nyumbani kwa Farao. Basi, kwa ajili yake, Farao alimfadhili Abramu, akampa kondoo, ng'ombe, punda dume, watumishi wa kiume na wa kike, punda jike na ngamia. Lakini Mwenyezi-Mungu akamtesa Farao na watu wote wa nyumba yake kwa mapigo makali kwa sababu ya Sarai, mkewe Abramu. Farao akamwita Abramu, akamwuliza, “Ni kitu gani hiki ulichonitendea? Mbona hukunijulisha kwamba Sarai ni mkeo? Kwa nini ulisema ni dada yako hata nikamchukua kuwa mke wangu? Basi, sasa mkeo ndiye huyo. Mchukue uende zako!” Kisha Farao aliwaamuru watu wake, nao wakamsindikiza Abramu njiani akiwa na mke wake na mali yake yote.