Mwanzo 12:9-20
Mwanzo 12:9-20 SRUV
Naye Abramu akasafiri, akazidi kwenda pande za kusini. Basi kulikuwa na njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa kali katika nchi. Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai. Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako. Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana. Wakuu wa Farao wakamwona, nao wakamsifu kwa Farao; basi yule mwanamke akapelekwa nyumbani mwa Farao. Naye akamtendea Abramu mema kwa ajili yake; naye alikuwa na kondoo na ng'ombe, na punda dume, na watumwa, na wajakazi, na punda majike, na ngamia. Lakini BWANA akampiga Farao na nyumba yake mapigo makuu, kwa ajili ya Sarai, mkewe Abramu. Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, Ni nini hili ulilonitenda? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo? Mbona ulisema, Huyo ni dada yangu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako. Farao akawaagiza watu kwa ajili yake, wakampeleka njiani, na mkewe, na kila alichokuwa nacho.