Ezekieli 44:1-9
Ezekieli 44:1-9 BHN
Yule mtu akanirudisha kwenye lango la nje linaloelekea mashariki, nje ya patakatifu, nalo lilikuwa limefungwa. Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Lango hili litaendelea kufungwa. Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kulitumia, kwa sababu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nimeingia kupitia lango hilo. Hivyo litadumu likiwa limefungwa. Hata hivyo, mkuu anayetawala anaweza kwenda huko na kula chakula chake kitakatifu mbele yangu. Ni lazima aingie na kutokea lango la chumba cha kuingilia.” Yule mtu akanipeleka mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kwa njia ya lango la kaskazini. Nilipoangalia, nikaona utukufu wa Mwenyezi-Mungu umeijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hapo nikaanguka kifudifudi. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Wewe mtu! Tia maanani mambo yote unayoona na kusikia. Nitakueleza kanuni na masharti ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Zingatia moyoni mwako kwa makini, ni watu gani wanaoruhusiwa kuingia na kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ni watu gani wamekatazwa kuingia humo. Utawaambia hao watu waasi wa Israeli, Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: Siwezi kuendelea kuyavumilia machukizo yenu yote. Mmeitia unajisi maskani yangu kwa kuruhusu waingie humo watu wasiotahiriwa, watu wasionitii mimi, wakati mafuta na damu vinatambikwa kwa ajili yangu. Hivyo, nyinyi watu wangu mmelivunja agano langu kwa machukizo yenu yote. Badala ya kutekeleza huduma ya vitu vyangu vitakatifu, mmeruhusu watu wa mataifa mengine kutekeleza huduma hiyo katika maskani yangu. Sasa, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hakuna mtu yeyote wa taifa geni, asiyetahiriwa au asiyenitii mimi, atakayeruhusiwa kuingia maskani yangu; hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli, hawataruhusiwa.