Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 44:1-9

Ezekieli 44:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

Yule mtu akanirudisha kwenye lango la nje linaloelekea mashariki, nje ya patakatifu, nalo lilikuwa limefungwa. Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Lango hili litaendelea kufungwa. Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kulitumia, kwa sababu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nimeingia kupitia lango hilo. Hivyo litadumu likiwa limefungwa. Hata hivyo, mkuu anayetawala anaweza kwenda huko na kula chakula chake kitakatifu mbele yangu. Ni lazima aingie na kutokea lango la chumba cha kuingilia.” Yule mtu akanipeleka mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kwa njia ya lango la kaskazini. Nilipoangalia, nikaona utukufu wa Mwenyezi-Mungu umeijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hapo nikaanguka kifudifudi. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Wewe mtu! Tia maanani mambo yote unayoona na kusikia. Nitakueleza kanuni na masharti ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Zingatia moyoni mwako kwa makini, ni watu gani wanaoruhusiwa kuingia na kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ni watu gani wamekatazwa kuingia humo. Utawaambia hao watu waasi wa Israeli, Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: Siwezi kuendelea kuyavumilia machukizo yenu yote. Mmeitia unajisi maskani yangu kwa kuruhusu waingie humo watu wasiotahiriwa, watu wasionitii mimi, wakati mafuta na damu vinatambikwa kwa ajili yangu. Hivyo, nyinyi watu wangu mmelivunja agano langu kwa machukizo yenu yote. Badala ya kutekeleza huduma ya vitu vyangu vitakatifu, mmeruhusu watu wa mataifa mengine kutekeleza huduma hiyo katika maskani yangu. Sasa, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hakuna mtu yeyote wa taifa geni, asiyetahiriwa au asiyenitii mimi, atakayeruhusiwa kuingia maskani yangu; hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli, hawataruhusiwa.

Ezekieli 44:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha akanirudisha kwa njia ya lango lile la nje, la mahali patakatifu lililoelekea upande wa mashariki; nalo lilikuwa limefungwa. BWANA akaniambia, Lango hili litafungwa, halitafunguliwa, wala mtu awaye yote hataingia kwa lango hili, kwa maana BWANA, Mungu wa Israeli, ameingia kwa hilo; basi kwa sababu hiyo litafungwa. Na mkuu, yeye ndiye atakayeketi ndani yake ale chakula mbele za BWANA; ataingia kwa njia ya ukumbi wa lango, naye atatoka kwa njia iyo hiyo. Kisha akanileta, kwa njia ya lango la upande wa kaskazini, mbele ya nyumba; nikaangalia, na tazama, huo utukufu wa BWANA uliijaza nyumba ya BWANA; nikaanguka kifudifudi. BWANA akaniambia, Mwanadamu, weka moyoni mwako, ukatazame kwa macho yako, ukasikie kwa masikio yako, maneno yote nitakayokuambia, katika habari ya kawaida zote za nyumba ya BWANA, na ya amri zake zote; nawe weka moyoni mwako maingilio ya nyumba, pamoja na matokeo yote ya mahali patakatifu. Nawe utawaambia waasi, yaani nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Enyi nyumba ya Israeli, machukizo yenu yote, na yakome, kuwa mmewaingiza wageni, ambao mioyo yao haikutahiriwa, wala miili yao haikutahiriwa, wawe ndani ya patakatifu pangu, wapatie unajisi, naam, nyumba yangu, mtoapo sadaka ya chakula changu, mafuta na damu; nao wameyavunja maagano yangu, juu ya machukizo yenu yote. Wala hamkuvilinda vitu vyangu vitakatifu bali mmejiwekea walinzi wa maagizo yangu, katika patakatifu pangu. Bwana MUNGU asema hivi; Hapana mgeni, ambaye moyo wake haukutahiriwa, wala mwili wake haukutahiriwa, atakayeingia patakatifu pangu, miongoni mwa wageni walio kati ya wana wa Israeli.

Ezekieli 44:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha akanirudisha kwa njia ya lango lile la nje, la mahali patakatifu lililoelekea upande wa mashariki; nalo lilikuwa limefungwa. BWANA akaniambia, Lango hili litafungwa, halitafunguliwa, wala mtu awaye yote hataingia kwa lango hili, kwa maana BWANA, Mungu wa Israeli, ameingia kwa hilo; basi kwa sababu hiyo litafungwa. Na mkuu, yeye ndiye atakayeketi ndani yake ale chakula mbele za BWANA; ataingia kwa njia ya ukumbi wa lango, naye atatoka kwa njia iyo hiyo. Kisha akanileta, kwa njia ya lango la upande wa kaskazini, mbele ya nyumba; nikaangalia, na tazama, huo utukufu wa BWANA uliijaza nyumba ya BWANA; nikaanguka kifudifudi. BWANA akaniambia, Mwanadamu, weka moyoni mwako, ukatazame kwa macho yako, ukasikie kwa masikio yako, maneno yote nitakayokuambia, katika habari ya kawaida zote za nyumba ya BWANA, na ya amri zake zote; nawe weka moyoni mwako maingilio ya nyumba, pamoja na matokeo yote ya mahali patakatifu. Nawe utawaambia waasi, yaani nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Enyi nyumba ya Israeli, katika machukizo yenu yote, na iwatoshe, kuwa mmewaingiza wageni, ambao mioyo yao haikutahiriwa, wala miili yao haikutahiriwa, wawe ndani ya patakatifu pangu, wapatie unajisi, naam, nyumba yangu, mtoapo sadaka ya chakula changu, mafuta na damu; nao wameyavunja maagano yangu, juu ya machukizo yenu yote. Wala hamkuvilinda vitu vyangu vitakatifu bali mmejiwekea walinzi wa kawaida zangu, katika patakatifu pangu. Bwana MUNGU asema hivi; Hapana mgeni, ambaye moyo wake haukutahiriwa, wala mwili wake haukutahiriwa, atakayeingia patakatifu pangu, miongoni mwa wageni walio kati ya wana wa Israeli.

Ezekieli 44:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo yule mtu akanirudisha mpaka kwenye lango la nje la mahali Patakatifu, lile linaloelekea upande wa mashariki, nalo lilikuwa limefungwa. BWANA akaniambia, “Lango hili litabaki limefungwa. Haliruhusiwi kufunguliwa, wala hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingilia kwenye lango hili. Litabaki limefungwa kwa sababu BWANA, Mungu wa Israeli, ameingia kwa kupitia lango hili. Yeye aliye mkuu peke yake ndiye anayeweza kukaa penye njia ya hilo lango na kula chakula mbele za BWANA. Itampasa aingie kwa njia hiyo ya lango la ukumbini na kutokea njia iyo hiyo.” Kisha yule mtu akanileta kwa njia ya lango la kaskazini mpaka mbele ya Hekalu. Nikatazama nami nikauona utukufu wa BWANA ukilijaza Hekalu la BWANA, nami nikaanguka kifudifudi. BWANA akaniambia, “Mwanadamu, angalia kwa uangalifu, usikilize kwa bidii na uzingatie kila kitu ninachokuambia kuhusu masharti yote yanayohusu Hekalu la BWANA. Uwe mwangalifu kuhusu wale wanaoruhusiwa hekaluni na wale wasioruhusiwa kuingia mahali patakatifu. Iambie nyumba ya kuasi ya Israeli, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Matendo yenu ya machukizo yatosha, ee nyumba ya Israeli! Zaidi ya matendo yenu yote ya machukizo, mmewaleta wageni wasiotahiriwa mioyo na miili katika patakatifu pangu, mkilinajisi Hekalu langu, huku mkinitolea chakula, mafuta ya wanyama na damu, nanyi mmevunja Agano langu. Badala ya kutimiza wajibu wenu kuhusiana na vitu vyangu vitakatifu, mmeweka watu wengine kuwa viongozi katika patakatifu pangu. Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Hakuna mgeni asiyetahiriwa moyo na mwilini anayeruhusiwa kuingia patakatifu pangu, wala hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli.