Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 43:1-12

Ezekieli 43:1-12 BHN

Kisha, yule mtu akanipeleka kwenye lango linaloelekea mashariki. Utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea upande wa mashariki. Pamoja nao kulikuwapo mshindo wa kuja kwake kama mshindo wa maji mengi, nchi ilingaa kwa utukufu wake. Maono hayo yalikuwa kama maono niliyoyaona Mungu alipokuja kuuangamiza mji wa Yerusalemu. Pia yalifanana na maono niliyoyaona karibu na mto Kebari. Nikaanguka kifudifudi. Nao utukufu wa Mwenyezi-Mungu uliingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa njia ya lango la mashariki. Kisha roho ya Mungu ikaninyanyua na kunipeleka kwenye uwanja wa ndani. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukiwa umeijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Yule mtu akiwa anasimama karibu nami, nilisikia mtu fulani akisema kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu; naye akaniambia, “Wewe mtu! Hapa ndipo mahali pa kiti changu cha enzi, mahali niwekapo nyayo za miguu yangu. Nitakaa miongoni mwa watu wa Israeli milele. Na Waisraeli hawatalitia unajisi jina langu, wao wenyewe, wala wafalme wao kwa kuziabudu sanamu au kuzika maiti za wafalme wao mahali hapa. Wafalme wao walijenga vizingiti na miimo ya ikulu zao karibu na vizingiti vya nguzo za hekalu langu, hivyo kati yangu na wao ulikuwa ni ukuta tu. Walilitia unajisi jina langu takatifu kwa machukizo yao waliyotenda, ndiyo maana nimewaangamiza kwa hasira yangu. Sasa na waache kuziabudu sanamu na waziondoe maiti za wafalme wao mbali nami, nami nitakaa miongoni mwao milele. “Sasa, ewe mtu, waeleze Waisraeli habari za nyumba ya Mungu na wajifunze ramani yake. Waaibike kutokana na machukizo yao waliyotenda. Wakiona aibu kutokana na matendo yao, waeleze ramani ya nyumba ya Mungu: Ramani yake yenyewe, milango ya kuingilia na kutokea, umbo lake lote, mipango ya kila kitu, kanuni zake na masharti yake. Waandikie hayo yote waziwazi ili waweze kuona yote yalivyopangwa na waweze kuzifuata kanuni na masharti yake. Hii ndiyo sheria kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Eneo lote linalozunguka nyumba ya Mwenyezi-Mungu juu ya mlima lazima liwe takatifu kabisa.”