Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 43:1-12

Ezekieli 43:1-12 NEN

Kisha yule mtu akanileta kwenye lango linaloelekea upande wa mashariki, nami nikaona utukufu wa Mungu wa Israeli ukija kutoka upande wa mashariki. Sauti yake ilikuwa kama ya ngurumo ya maji yaendayo kasi, nayo nchi ikangʼaa kwa utukufu wake. Maono niliyoyaona yalikuwa kama maono yale niliyokuwa nimeyaona wakati Mungu alipokuja kuangamiza mji na kama maono niliyokuwa nimeyaona kando ya Mto wa Kebari, nami nikaanguka kifudifudi. Utukufu wa BWANA ukaingia hekaluni kwa kupitia lango linaloelekea upande wa mashariki. Kisha Roho akanichukua na kunileta katika ule ua wa ndani, nao utukufu wa BWANA ulilijaza Hekalu. Wakati yule mtu akiwa amesimama kando yangu, nilisikia mtu mmoja akisema nami kutoka ndani ya Hekalu. Akasema, “Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi na mahali pa kuweka nyayo za miguu yangu. Hapa ndipo nitakapoishi miongoni mwa Waisraeli milele. Kamwe nyumba ya Israeli hawatalinajisi tena Jina langu takatifu, yaani, wao wala wafalme wao, kwa ukahaba wao na kwa sanamu zao zisizokuwa na uhai za wafalme wao katika mahali pao pa juu pa kuabudia miungu. Walipoweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu na miimo yao ya milango karibu na miimo yangu, pakiwa na ukuta tu kati yangu na wao, walilinajisi Jina langu takatifu kwa matendo yao ya machukizo. Kwa sababu hiyo niliwaangamiza kwa hasira yangu. Basi sasa na waweke mbali nami ukahaba wao na sanamu za wafalme wao zisizo na uhai, nami nitakaa miongoni mwao milele. “Mwanadamu, elezea hilo Hekalu kwa watu wa Israeli, ili wapate kuona aibu kwa ajili ya dhambi zao. Wao na wapime hicho kielelezo. Wakishaona aibu kwa ajili ya yale yote waliyotenda, wafahamishe kielelezo cha hilo Hekalu, yaani mpangilio wake, maingilio yake ya kutoka na kuingia, kielelezo chake chote, na masharti yake yote na sheria zake zote. Yaandike haya mbele yao ili wapate kuwa waaminifu kwa hicho kielelezo chake na kufuata masharti yake yote. “Hii ndiyo sheria ya Hekalu: Eneo lote linalozunguka Hekalu juu ya mlima litakuwa takatifu kuliko yote. Hii ndiyo sheria ya Hekalu.