Ezekieli 43:1-12
Ezekieli 43:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha akanileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki; na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling’aa kwa utukufu wake. Na maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona nilipokuja kuuharibu mji; nayo maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona karibu na mto wa Kebari; nikaanguka kifudifudi. Na huo utukufu wa BWANA ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki. Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa BWANA uliijaza nyumba. Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami. Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele; na nyumba ya Israeli hawatalinajisi jina langu takatifu tena, wao, wala wafalme wao, kwa mambo yao ya kikahaba, na kwa mizoga ya wafalme wao, katika mahali pao pa juu; kwa kuweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu; na mwimo wao karibu na mwimo wangu; tena palikuwa na ukuta tu kati ya mimi na wao; nao wamelinajisi jina langu takatifu kwa machukizo yao waliyoyatenda; basi, kwa sababu hiyo, nimewakomesha katika hasira yangu. Basi sasa wayaondoe mambo yao ya kikahaba, na mizoga ya wafalme wao, yawe mbali nami, nami nitakaa kati yao milele. Na wewe, mwanadamu, waonyeshe wana wa Israeli nyumba hii, ili wayatahayarikie maovu yao; na waipime hesabu yake. Na ikiwa wameyatahayarikia yote waliyoyatenda, waonyeshe umbo la nyumba, na namna yake, na matokeo yake, na maingilio yake, na maumbo yake yote, na maagizo yake yote, na kawaida zake zote, na sheria zake zote, ukayaandike machoni pao; ili walishike umbo lake lote, na maagizo yake, na kuyatenda. Hii ndiyo sheria ya nyumba; juu ya kilele cha mlima, mpaka wake wote pande zote patakuwa patakatifu sana. Tazama, hii ndiyo sheria ya nyumba.
Ezekieli 43:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, yule mtu akanipeleka kwenye lango linaloelekea mashariki. Utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea upande wa mashariki. Pamoja nao kulikuwapo mshindo wa kuja kwake kama mshindo wa maji mengi, nchi ilingaa kwa utukufu wake. Maono hayo yalikuwa kama maono niliyoyaona Mungu alipokuja kuuangamiza mji wa Yerusalemu. Pia yalifanana na maono niliyoyaona karibu na mto Kebari. Nikaanguka kifudifudi. Nao utukufu wa Mwenyezi-Mungu uliingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa njia ya lango la mashariki. Kisha roho ya Mungu ikaninyanyua na kunipeleka kwenye uwanja wa ndani. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukiwa umeijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Yule mtu akiwa anasimama karibu nami, nilisikia mtu fulani akisema kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu; naye akaniambia, “Wewe mtu! Hapa ndipo mahali pa kiti changu cha enzi, mahali niwekapo nyayo za miguu yangu. Nitakaa miongoni mwa watu wa Israeli milele. Na Waisraeli hawatalitia unajisi jina langu, wao wenyewe, wala wafalme wao kwa kuziabudu sanamu au kuzika maiti za wafalme wao mahali hapa. Wafalme wao walijenga vizingiti na miimo ya ikulu zao karibu na vizingiti vya nguzo za hekalu langu, hivyo kati yangu na wao ulikuwa ni ukuta tu. Walilitia unajisi jina langu takatifu kwa machukizo yao waliyotenda, ndiyo maana nimewaangamiza kwa hasira yangu. Sasa na waache kuziabudu sanamu na waziondoe maiti za wafalme wao mbali nami, nami nitakaa miongoni mwao milele. “Sasa, ewe mtu, waeleze Waisraeli habari za nyumba ya Mungu na wajifunze ramani yake. Waaibike kutokana na machukizo yao waliyotenda. Wakiona aibu kutokana na matendo yao, waeleze ramani ya nyumba ya Mungu: Ramani yake yenyewe, milango ya kuingilia na kutokea, umbo lake lote, mipango ya kila kitu, kanuni zake na masharti yake. Waandikie hayo yote waziwazi ili waweze kuona yote yalivyopangwa na waweze kuzifuata kanuni na masharti yake. Hii ndiyo sheria kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Eneo lote linalozunguka nyumba ya Mwenyezi-Mungu juu ya mlima lazima liwe takatifu kabisa.”
Ezekieli 43:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha akanileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki; na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling'aa kwa utukufu wake. Na maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona nilipokuja kuuharibu mji; nayo maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona karibu na mto wa Kebari; nikaanguka kifudifudi. Na huo utukufu wa BWANA ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki. Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka katika ua wa ndani; na tazama, utukufu wa BWANA uliijaza nyumba. Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami. Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele; na nyumba ya Israeli hawatalinajisi jina langu takatifu tena, wao, wala wafalme wao, kwa mambo yao ya kikahaba, na kwa mizoga ya wafalme wao, katika mahali pao pa juu; kwa kuweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu; na mwimo wao karibu na mwimo wangu; tena palikuwa na ukuta tu kati ya mimi na wao; nao wamelinajisi jina langu takatifu kwa machukizo yao waliyoyatenda; basi, kwa sababu hiyo, nimewaangamiza katika hasira yangu. Basi sasa wayaondoe mambo yao ya kikahaba, na mizoga ya wafalme wao, yawe mbali nami, nami nitakaa kati yao milele. Na wewe, mwanadamu, waoneshe wana wa Israeli nyumba hii, ili wayatahayarikie maovu yao; na waipime hesabu yake. Na ikiwa wameyatahayarikia yote waliyoyatenda, waoneshe umbo la nyumba, na namna yake, na matokeo yake, na maingilio yake, na maumbo yake yote, na maagizo yake yote, na kawaida zake zote, na sheria zake zote, ukayaandike machoni pao; ili walishike umbo lake lote, na maagizo yake, na kuyatenda. Hii ndiyo sheria ya nyumba; juu ya kilele cha mlima, mpaka wake wote pande zote patakuwa patakatifu sana. Tazama, hii ndiyo sheria ya nyumba.
Ezekieli 43:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha yule mtu akanileta kwenye lango linaloelekea upande wa mashariki, nami nikaona utukufu wa Mungu wa Israeli ukija kutoka upande wa mashariki. Sauti yake ilikuwa kama ya ngurumo ya maji yaendayo kasi, nayo nchi ikangʼaa kwa utukufu wake. Maono niliyoyaona yalikuwa kama maono yale niliyokuwa nimeyaona wakati Mungu alipokuja kuangamiza mji na kama maono niliyokuwa nimeyaona kando ya Mto wa Kebari, nami nikaanguka kifudifudi. Utukufu wa BWANA ukaingia hekaluni kwa kupitia lango linaloelekea upande wa mashariki. Kisha Roho akanichukua na kunileta katika ule ua wa ndani, nao utukufu wa BWANA ulilijaza Hekalu. Wakati yule mtu akiwa amesimama kando yangu, nilisikia mtu mmoja akisema nami kutoka ndani ya Hekalu. Akasema, “Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi na mahali pa kuweka nyayo za miguu yangu. Hapa ndipo nitakapoishi miongoni mwa Waisraeli milele. Kamwe nyumba ya Israeli hawatalinajisi tena Jina langu takatifu, yaani, wao wala wafalme wao, kwa ukahaba wao na kwa sanamu zao zisizokuwa na uhai za wafalme wao katika mahali pao pa juu pa kuabudia miungu. Walipoweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu na miimo yao ya milango karibu na miimo yangu, pakiwa na ukuta tu kati yangu na wao, walilinajisi Jina langu takatifu kwa matendo yao ya machukizo. Kwa sababu hiyo niliwaangamiza kwa hasira yangu. Basi sasa na waweke mbali nami ukahaba wao na sanamu za wafalme wao zisizo na uhai, nami nitakaa miongoni mwao milele. “Mwanadamu, elezea hilo Hekalu kwa watu wa Israeli, ili wapate kuona aibu kwa ajili ya dhambi zao. Wao na wapime hicho kielelezo. Wakishaona aibu kwa ajili ya yale yote waliyotenda, wafahamishe kielelezo cha hilo Hekalu, yaani mpangilio wake, maingilio yake ya kutoka na kuingia, kielelezo chake chote, na masharti yake yote na sheria zake zote. Yaandike haya mbele yao ili wapate kuwa waaminifu kwa hicho kielelezo chake na kufuata masharti yake yote. “Hii ndiyo sheria ya Hekalu: Eneo lote linalozunguka Hekalu juu ya mlima litakuwa takatifu kuliko yote. Hii ndiyo sheria ya Hekalu.