Ezekieli 24:15-27
Ezekieli 24:15-27 BHN
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Tazama, kwa pigo moja nitakuondolea mpenzi wako. Lakini usiomboleze, wala kulia, wala kutoa machozi. Utasononeka, lakini sio kwa sauti. Hutamfanyia matanga huyo aliyekufa. Vaa viatu vyako na kuvaa kilemba; usiufunike uso wako wala kula chakula cha matanga.” Basi, asubuhi nilizungumza na watu, na jioni mke wangu akafariki. Na kesho yake asubuhi, nilifanya kama nilivyoamriwa. Watu wakaniuliza: “Je, jambo hili unalofanya lamaanisha nini kwetu?” Nikawajibu, “Mwenyezi-Mungu aliniagiza niwaambie nyinyi Waisraeli kwamba Mwenyezi-Mungu ataitia unajisi maskani yake, hiyo nyumba ambayo ni fahari ya ukuu wenu, na ambayo mnafurahi sana kuiona. Nao watoto wenu, wa kiume kwa wa kike, mliowaacha nyuma watauawa kwa upanga. Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya. Hamtazifunika nyuso zenu wala kula chakula cha matanga. Mtavaa vilemba vyenu na viatu miguuni; hamtaomboleza, wala kulia. Kutokana na maovu yenu, mtadhoofika na kusononeka, kila mtu na mwenzake. Nami Ezekieli nitakuwa ishara kwenu: Mtafanya kila kitu kama nilivyotenda. Wakati mambo hayo yatakapotukia, mtatambua kuwa yeye ndiye Bwana Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Wewe mtu! Siku ile nitakapoondoa kwao hicho ambacho ni tegemeo lao, na sababu ya shangwe yao, mahali ambapo wanapenda sana kupaona, nitawaondoa watoto wao wa kiume na wa kike. Siku hiyo, mtu atakayeokoka atakuja kukupasha habari hizo. Siku hiyohiyo, utaacha kuwa bubu, nawe utaweza kuongea naye. Kwa hiyo wewe utakuwa ishara kwao, nao watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”