Ezekieli 24:15-27
Ezekieli 24:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Tazama, kwa pigo moja nitakuondolea mpenzi wako. Lakini usiomboleze, wala kulia, wala kutoa machozi. Utasononeka, lakini sio kwa sauti. Hutamfanyia matanga huyo aliyekufa. Vaa viatu vyako na kuvaa kilemba; usiufunike uso wako wala kula chakula cha matanga.” Basi, asubuhi nilizungumza na watu, na jioni mke wangu akafariki. Na kesho yake asubuhi, nilifanya kama nilivyoamriwa. Watu wakaniuliza: “Je, jambo hili unalofanya lamaanisha nini kwetu?” Nikawajibu, “Mwenyezi-Mungu aliniagiza niwaambie nyinyi Waisraeli kwamba Mwenyezi-Mungu ataitia unajisi maskani yake, hiyo nyumba ambayo ni fahari ya ukuu wenu, na ambayo mnafurahi sana kuiona. Nao watoto wenu, wa kiume kwa wa kike, mliowaacha nyuma watauawa kwa upanga. Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya. Hamtazifunika nyuso zenu wala kula chakula cha matanga. Mtavaa vilemba vyenu na viatu miguuni; hamtaomboleza, wala kulia. Kutokana na maovu yenu, mtadhoofika na kusononeka, kila mtu na mwenzake. Nami Ezekieli nitakuwa ishara kwenu: Mtafanya kila kitu kama nilivyotenda. Wakati mambo hayo yatakapotukia, mtatambua kuwa yeye ndiye Bwana Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Wewe mtu! Siku ile nitakapoondoa kwao hicho ambacho ni tegemeo lao, na sababu ya shangwe yao, mahali ambapo wanapenda sana kupaona, nitawaondoa watoto wao wa kiume na wa kike. Siku hiyo, mtu atakayeokoka atakuja kukupasha habari hizo. Siku hiyohiyo, utaacha kuwa bubu, nawe utaweza kuongea naye. Kwa hiyo wewe utakuwa ishara kwao, nao watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”
Ezekieli 24:15-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, tazama, ninakuondolea kwa pigo moja tunu, mteule wa macho yako; walakini hutaomboleza wala kulia, wala yasichuruzike machozi yako. Piga kite lakini si kwa sauti ya kusikiwa; usifanye matanga kwa ajili yake yeye aliyekufa; jipige kilemba chako, ukavae viatu vyako, wala usiifunike midomo yako, wala usile chakula cha watu. Basi nilisema na watu asubuhi, na jioni mke wangu akafa; nami kesho yake asubuhi nilifanya kama nilivyoagizwa. Watu hao wakaniambia, Je! Hutaki kutuambia maana ya mambo haya kwetu, hata umefanya kama vile ufanyavyo. Nikawaambia, Neno la BWANA lilinijia, kusema, Uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Angalieni, nitapatia unajisi patakatifu pangu, fahari ya uwezo wenu, mahali pa kutamaniwa na macho yenu, ambapo roho zenu zinapahurumia na wana wenu na binti zenu, mliowaacha nyuma, wataanguka kwa upanga. Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya; hamtaifunika midomo yenu, wala kula chakula cha watu. Na vilemba vyenu vitakuwa juu ya vichwa vyenu, na viatu vyenu miguuni mwenu; hamtaomboleza wala kulia; lakini mtafifia katika maovu yenu, na kusikitika kila mtu pamoja na mwenziwe. Basi ndivyo Ezekieli atakavyokuwa ishara kwenu; ninyi mtatenda sawasawa na yote aliyoyatenda yeye; litakapokuja jambo hili, ndipo mtakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU. Nawe, mwanadamu, je! Haitakuwa hivi katika siku hiyo nitakapowaondolea nguvu zao, na furaha ya utukufu wao, na kilichotamaniwa na macho yao, ambacho walikiinulia mioyo yao, watoto wao wa kiume na watoto wao wa kike, kwamba katika siku iyo hiyo yeye atakayeokoka atakuja kwako, akusikize jambo hili kwa masikio yako? Siku hiyo kinywa chako kitafumbuliwa kwake aliyeokoka, nawe utasema; hutakuwa bubu tena; ndivyo utakavyokuwa ishara kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Ezekieli 24:15-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, tazama, ninakuondolea kwa pigo moja tunu, mteule wa macho yako; walakini hutaomboleza wala kulia, wala yasichuruzike machozi yako. Ugua lakini si kwa sauti ya kusikiwa; usifanye matanga kwa ajili yake yeye aliyekufa; jipige kilemba chako, ukavae viatu vyako, wala usiifunike midomo yako, wala usile chakula cha watu. Basi nalisema na watu asubuhi, na jioni mke wangu akafa; nami nalifanya asubuhi kama nilivyoagizwa. Watu hao wakaniambia, Je! Hutaki kutuambia maana ya mambo haya kwetu, hata umefanya kama vile ufanyavyo. Nikawaambia, Neno la BWANA lilinijia, kusema, Uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Angalieni, nitapatia unajisi patakatifu pangu, fahari ya uwezo wenu, mahali pa kutamaniwa na macho yenu, ambapo roho zenu zinapahurumia na wana wenu na binti zenu, mliowaacha nyuma, wataanguka kwa upanga. Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya; hamtaifunika midomo yenu, wala kula chakula cha watu. Na vilemba vyenu vitakuwa juu ya vichwa vyenu, na viatu vyenu miguuni mwenu; hamtaomboleza wala kulia; lakini mtafifia katika maovu yenu, na kuugua kila mtu pamoja na mwenziwe. Basi ndivyo Ezekieli atakavyokuwa ishara kwenu; ninyi mtatenda sawasawa na yote aliyoyatenda yeye; litakapokuja jambo hili, ndipo mtakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU. Nawe, mwanadamu, je! Haitakuwa hivi katika siku hiyo nitakapowaondolea nguvu zao, na furaha ya utukufu wao, na kilichotamaniwa na macho yao, ambacho walikiinulia mioyo yao, wana wao na binti zao, kwamba katika siku iyo hiyo yeye atakayeokoka atakuja kwako, akusikize jambo hili kwa masikio yako? Siku hiyo kinywa chako kitafumbuliwa kwake aliyeokoka, nawe utasema; hutakuwa bubu tena; ndivyo utakavyokuwa ishara kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Ezekieli 24:15-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, kwa pigo moja nakaribia kukuondolea kile kilicho furaha ya macho yako. Lakini usiomboleze au kulia wala kudondosha machozi yoyote. Lia kwa uchungu kimya kimya usimwombolezee mtu aliyekufa. Jifunge kilemba chako na uvae viatu vyako miguuni mwako, usifunike sehemu ya chini ya uso wako, wala usile vyakula vya kawaida vya wakati wa matanga.” Hivyo nikanena na watu asubuhi na jioni mke wangu akafa. Asubuhi yake nilifanya kama nilivyoamriwa. Ndipo watu wakaniuliza, “Je, jambo hili unalofanya linamaanisha nini kwetu?” Kwa hiyo nikawaambia, “Neno la BWANA lilinijia kusema: ‘Sema na nyumba ya Israeli. Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ninakaribia kupatia unajisi mahali pangu patakatifu, ngome ambayo ndani yake mnaona fahari, furaha ya macho yenu, kitu mnachokipenda. Wana wenu na binti zenu mliowaacha nyuma wataanguka kwa upanga. Nanyi mtafanya kama nilivyofanya. Hamtafunika sehemu ya chini ya nyuso zenu wala hamtakula vyakula vya kawaida vya waombolezaji. Mtajifunga vilemba vichwani mwenu na kuvaa viatu vyenu miguuni mwenu. Hamtaomboleza au kulia, lakini mtadhoofika kwa sababu ya dhambi zenu na kulia kwa uchungu kila mtu na mwenzake. Ezekieli atakuwa ishara kwenu, mtafanya kama yeye alivyofanya. Wakati jambo hili litakapotokea, mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA Mwenyezi.’ “Nawe, mwanadamu, siku ile nitakapoondoa ngome yao iliyo furaha yao na utukufu wao, kitu cha kupendeza macho yao, kile kilicho shauku ya mioyo yao, wana wao na binti zao vilevile, siku hiyo atakayetoroka atakuja kuwapasha habari. Katika siku ile kinywa chako kitamfumbukia yeye aliyenusurika, nawe utaongea wala hutanyamaza tena. Hivyo wewe utakuwa ishara kwao, nao watajua kuwa Mimi ndimi BWANA.”