Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 24:1-14

Ezekieli 24:1-14 BHN

Mnamo siku ya kumi, mwezi wa kumi, mwaka wa tisa tangu kuhamishwa kwetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Andika tarehe ya siku ya leo, maana hii ni siku ambapo mfalme wa Babuloni anaanza kuuzingira mji wa Yerusalemu. Wape mfano hao watu wangu waasi na kuwaambia kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Kiweke chungu juu ya meko, ukakijaze maji pia. Tia humo vipande vya nyama, vipande vizuri vya mapaja na mabega. Kijaze pia mifupa mizuri. Tumia nyama nzuri ya kondoo, panga kuni chini ya chungu, chemsha vipande vya nyama na mifupa, vyote uvichemshe vizuri. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wake mji wa mauaji! Mji huo ni kama chungu chenye kutu, ambacho kutu yake haiwezi kutoka! Vipande vya nyama ndani yake hutolewa kimojakimoja bila kuchaguliwa. Mauaji yamo humo mjini; damu yenyewe haikumwagwa udongoni ifunikwe na vumbi, ila ilimwagwa mwambani. Damu hiyo nimeiacha huko mwambani ili isifunikwe, nipate kuamsha ghadhabu yangu na kulipiza kisasi. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wake mji wa mauaji! Mimi nitarundika rundo kubwa la kuni. Nitaleta magogo ya kuni na kuwasha moto. Nitachemsha nyama vizuri sana. Nitachemsha na kukausha mchuzi, na mifupa nitaiunguza! Hicho chungu kitupu nitakiweka juu ya makaa kipate moto sana, shaba yake ipate moto, uchafu wake uyeyushwe na kutu iunguzwe. Lakini najisumbua bure; kutu yake nene haitoki hata kwa moto. Ewe Yerusalemu, matendo yako machafu yamekutia unajisi. Ingawa nilijaribu kuutakasa, wenyewe ulibaki najisi. Basi, hutatakasika tena mpaka nitakapoitosheleza hasira yangu juu yako. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Jambo hilo litakamilika; mimi nitalitenda. Sitaghairi jambo hilo wala kukuonea huruma. Nitakuadhibu kulingana na mwenendo na matendo yako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”