Ezekieli 24:1-14
Ezekieli 24:1-14 NEN
Katika mwaka wa tisa, mwezi wa kumi, siku ya kumi, neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, weka kumbukumbu ya tarehe hii, tarehe hii hasa, kwa kuwa mfalme wa Babeli ameuzingira mji wa Yerusalemu kwa jeshi siku hii ya leo. Iambie nyumba hii ya kuasi fumbo, na uwaambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Teleka sufuria jikoni; iteleke na umimine maji ndani yake, Weka vipande vya nyama ndani yake, vipande vyote vizuri, vya paja na vya bega. Ijaze hiyo sufuria kwa mifupa hii mizuri; chagua yule aliye bora wa kundi la kondoo. Panga kuni chini ya sufuria kwa ajili ya mifupa; chochea mpaka ichemke na uitokose hiyo mifupa ndani yake. “ ‘Kwa kuwa hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Ole wa mji umwagao damu, ole wa sufuria ambayo sasa ina ukoko ndani yake, ambayo ukoko wake hautoki. Kipakue kipande baada ya kipande, bila kuvipigia kura. “ ‘Kwa kuwa damu aliyoimwaga ipo katikati yake: huyo mwanamke aliimwaga juu ya mwamba ulio wazi; hakuimwaga kwenye ardhi, ambako vumbi lingeifunika. Kuchochea ghadhabu na kulipiza kisasi, nimemwaga damu yake juu ya mwamba ulio wazi, ili isifunikwe. “ ‘Kwa hiyo, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Ole wa mji umwagao damu! Mimi nami nitalundikia kuni nyingi. Kwa hiyo lundika kuni na uwashe moto. Pika hiyo nyama vizuri, changanya viungo ndani yake, na uiache mifupa iungue kwenye moto. Kisha teleka sufuria tupu kwenye makaa mpaka iwe na moto sana na shaba yake ingʼae, ili uchafu wake upate kuyeyuka na ukoko wake upate kuungua na kuondoka. Imezuia juhudi zote, ukoko wake mwingi haujaondoka, hata ikiwa ni kwa moto. “ ‘Sasa uchafu wako ni uasherati wako. Kwa sababu nilijaribu kukutakasa lakini haikuwezekana kutakaswa kutoka kwenye huo uchafu wako, hutatakasika tena mpaka ghadhabu yangu dhidi yako iwe imepungua. “ ‘Mimi BWANA nimesema, wakati umewadia wa mimi kutenda. Mimi sitazuia, mimi sitaona huruma wala sitapunguza hasira yangu, Utahukumiwa sawasawa na mwenendo na matendo yako, asema BWANA Mwenyezi.’ ”