Ezekieli 16:44-63
Ezekieli 16:44-63 BHN
“Ewe Yerusalemu! Mtu akitaka kutumia methali juu yako atasema: ‘Kama mama alivyo ndivyo alivyo binti yake.’ Kweli wewe ni mtoto wa mama aliyemchukia mumewe na watoto wake; wewe ni sawa na dada zako waliowachukia waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti na baba yako alikuwa Mwamori. Dada yako mkubwa ni Samaria, aliyekaa upande wako wa kaskazini mwako pamoja na binti zake. Dada yako mdogo ni Sodoma, aliyekaa upande wako wa kusini pamoja na binti zake. Lakini wewe hukutosheka kufuata mienendo yao au kutenda sawa na machukizo yao. Kwa muda mfupi tu ulipotoka kuliko walivyopotoka wao katika mienendo yako yote. Kweli naapa kwa nafsi yangu, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu kuwa, dada yako Sodoma na binti zake, hawakufanya maovu kama yale uliyotenda wewe na binti zako. Kosa la dada yako Sodoma, lilikuwa hili: Yeye pamoja na binti zake walipokuwa na chakula na fanaka tele, walianza kujivuna, wakaacha kuwasaidia maskini na fukara. Walijivuna, wakafanya machukizo mbele yangu. Kwa hiyo niliwaangamiza mara tu nilipoyaona hayo. Naye Samaria kwa kweli hakutenda hata nusu ya dhambi zako. Wewe umefanya machukizo mengi kuliko wao. Ukilinganisha maovu yako na ya dada zako, maovu yao si kitu! Wewe utaibeba aibu yako kabisa! Dhambi zako ni mbaya zaidi kuliko za dada zako, kiasi cha kuwafanya dada zako na dhambi zao waonekane hawana hatia. Basi, ona aibu na kubeba fedheha yako, maana umewafanya dada zako waonekane hawana hatia. “Nitawarudishia Sodoma na Samaria pamoja na binti zao fanaka yao ya awali. Nawe pia nitakufanikisha miongoni mwao, ili ubebe aibu yako na kuona haya, kwa sababu ya mambo yote uliyotenda, ndipo kwa hali yako hiyo dada zako watajiona kwamba wao ni afadhali. Dada zako, Sodoma na Samaria, pamoja na binti zao watairudia hali yao ya hapo awali. Hata wewe na binti zako mtairudia hali yenu. Kwa majivuno yako ulimdharau dada yako Sodoma. Je, hukufanya hivyo kabla uovu wako haujafichuliwa? Sasa umekuwa kama Sodoma. Umekuwa kitu cha dhihaka mbele ya binti za Edomu na jirani zake wote, na binti za Wafilisti jirani zako ambao walikuchukia. Adhabu ya uchafu wa tabia na machukizo yako utaibeba wewe mwenyewe. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Naam! Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitakutenda wewe Yerusalemu kama unavyostahili. Wewe umekidharau kiapo chako, ukavunja na lile agano. Lakini mimi nitalikumbuka agano langu nililoagana nawe katika siku za ujana wako. Nitafanya nawe agano la milele. Nawe utakumbuka mienendo yako na kuona aibu wakati nitakapokupa dada zako, mkubwa na mdogo, kama binti zako, ingawa si kwa sababu ya agano kati yangu na wewe. Mimi nitafanya agano nawe, nawe utatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nitakusamehe kila kitu ulichotenda. Nawe utakapokumbuka hayo yote uliyotenda utashangaa na kunyamaza kwa aibu wala hutathubutu kusema tena. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”