Ezekieli 16:44-63
Ezekieli 16:44-63 SRUV
Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia mithali hii kinyume chako, akisema, Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake. Wewe u binti ya mama yako, amchukiaye mume wake na watoto wake; nawe u dada wa dada zako, waliowachukia waume zao na watoto wao; mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako Mwamori. Na dada yako mkubwa ni Samaria, akaaye mkono wako wa kushoto, yeye na binti zake; na dada yako mdogo, akaaye mkono wako wa kulia, ni Sodoma na binti zake. Lakini hukuenda katika njia zao, na hukutenda kulingana na machukizo yao; lakini kwa kitambo kidogo ulikuwa umepotoka kuliko wao katika njia zako zote. Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, Sodoma, dada yako, yeye na binti zake, hawakutenda kama wewe ulivyotenda, wewe na binti zako. Tazama, uovu wa dada yako, Sodoma, ulikuwa huu; kiburi, na kushiba chakula, na kufanikiwa, hayo yalikuwa ndani yake na binti zake; lakini hukuwasaidia maskini na wahitaji. Nao walijivuna, wakafanya machukizo mbele zangu; kwa sababu hiyo niliwaondoa hapo nilipoyaona. Samaria naye hakutenda nusu ya dhambi zako; bali wewe umeyaongeza machukizo yako zaidi ya hao, nawe umewapa haki dada zako kwa machukizo yako yote uliyoyatenda. Wewe nawe, ichukue aibu yako mwenyewe, kwa kuwa umetoa hukumu juu ya dada zako; kwa dhambi zako ulizozitenda, zilizochukiza kuliko hao, wao wana haki kuliko wewe; naam, ufedheheke wewe nawe, ukaichukue aibu yako, kwa kuwa umewapa haki dada zako. Nami nitawarudisha watu wao waliofungwa; wafungwa wa Sodoma na binti zake, na wafungwa wa Samaria na binti zake na wafungwa wako waliofungwa kati yao; upate kuichukua aibu yako mwenyewe, na kutahayari, kwa sababu ya mambo yote uliyoyatenda, kwa kuwa umekuwa faraja kwao. Na dada zako, Sodoma na binti zake, watairudia hali yao ya kwanza, na Samaria na binti zake watairudia hali yao ya kwanza, na wewe na binti zako mtairudia hali yenu ya kwanza. Kwa maana dada yako, Sodoma, hakutajwa kwa kinywa chako katika siku ya kiburi chako; kabla uovu wako haujafunuliwa bado, kama vile wakati ule walipokutukana binti za Shamu, na wale wote waliomzunguka, binti za Wafilisti wanaokudharau pande zote. Yakupasa kupata adhabu ya uasherati wako, na machukizo yako, asema BWANA. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitakutenda vile vile kama ulivyotenda, uliyekidharau kiapo kwa kulivunja agano. Walakini nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe, katika siku za ujana wako, nami nitaweka imara agano la milele pamoja nawe. Hapo ndipo utakapozikumbuka njia zako, na kutahayarika, hapo utakapowakaribisha dada zako, walio wakubwa wako na wadogo wako; nami nitakupa hao wawe binti zako, lakini si kwa agano lako. Nami nitaweka imara agano langu nawe; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aibu yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda, asema Bwana MUNGU.