Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 13:1-16

Ezekieli 13:1-16 BHN

Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, wakaripie manabii wa Israeli wanaotangaza mambo ambayo wameyafikiria wao wenyewe. Waambie wasikilize yale ambayo mimi Mwenyezi-Mungu ninasema. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Ole wenu manabii wapumbavu mnaofuata mawazo yenu wenyewe na maono yenu wenyewe! Manabii wenu, enyi Waisraeli ni kama mbweha wanaopitapita katika magofu. Hawakwenda kulinda sehemu zile za kuta zilizobomoka wala hawajengi kuta mpya ili Waisraeli waweze kujilinda wakati wa vita siku ile ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nimeiweka. Maono yao ni ya uongo mtupu na wanachotabiri ni udanganyifu mtupu. Hudai kwamba wanasema kwa niaba yangu mimi Mwenyezi-Mungu, lakini mimi sikuwatuma; kisha wananitazamia nitimize wanayosema. Basi, nawaulizeni: Je, maono yenu si uongo mtupu na utabiri wenu udanganyifu? Nyinyi mnadai kwamba mnasema kwa jina langu hali mimi sijaongea nanyi kamwe! “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa kuwa maneno yenu ni udanganyifu na maono yenu ni ya uongo mtupu, basi, mimi nitapambana nanyi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitanyosha mkono wangu dhidi yenu nyinyi manabii mnaotoa maono ya uongo na kutabiri udanganyifu mtupu. Watu wangu watakapokutanika kuamua mambo, nyinyi hamtakuwapo. Wala hamtakuwa katika orodha ya watu wa Israeli na hamtaingia katika nchi ya Israeli; ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu. Manabii hao wanawapotosha watu wangu na kuwaambia ‘Kuna amani’, wakati hakuna amani. Watu wangu wanajenga ukuta usiofaa, nao wanaupaka chokaa! Sasa waambie hao manabii wanaopaka chokaa ukuta huo kwamba itanyesha mvua kubwa ya mawe na dhoruba na ukuta huo utaanguka. Je, utakapoanguka, watu hawatawauliza: ‘Na ile chokaa mlioupaka iko wapi?’ Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Kwa ghadhabu yangu nitazusha upepo wa dhoruba na mvua nyingi ya mawe, navyo vitauangusha ukuta huo. Nitaubomolea mbali huo ukuta mlioupaka chokaa, na msingi wake utakuwa wazi. Ukuta huo ukianguka, mtaangamia chini yake. Ndipo mtakapotambua mimi ni Mwenyezi-Mungu. Hasira yangu yote nitaimalizia juu ya ukuta huo na juu ya hao walioupaka chokaa. Nanyi mtaambiwa: Ukuta haupo tena, wala walioupaka rangi hawapo; mwisho wa manabii wa Israeli waliotabiri mema juu ya Yerusalemu na kuona maono ya amani hali hakuna amani. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.