Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 13:1-16

Ezekieli 13:1-16 SRUV

Kisha neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lolote! Ee Israeli, manabii wako wamekuwa kama mbweha, mahali palipo ukiwa. Hamkupanda kwenda mahali palipobomolewa, wala hamkuitengenezea nyumba ya Israeli boma, wapate kusimama vitani katika siku ya BWANA. Wameona ubatili, na uganga wa uongo, hao wasemao, BWANA asema; lakini BWANA hakuwatuma; nao wamewapa watu tumaini ya kuwa neno lile litatimizwa. Je! Hamkuona maono ya bure, hamkunena ubashiri wa uongo? Nanyi mwasema, BWANA asema; ila mimi sikusema neno. Basi tazama, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu mmenena ubatili, na kuona uongo, basi, kwa sababu hiyo, mimi ni juu yenu, asema Bwana MUNGU. Na mkono wangu utakuwa juu ya manabii wanaoona ubatili, na kutabiri uongo; hawatakuwa katika mashauri ya watu wangu, wala hawataandikwa katika maandiko ya nyumba ya Israeli, wala hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU. Kwa sababu hiyo, kwa sababu wameshawishi watu wangu, wakisema, Amani; wala hapana amani; na mtu mmoja ajengapo ukuta, tazama, waupaka chokaa isiyokorogwa vema; basi waambie hao wanaoupaka ukuta chokaa isiyokorogwa vema, ya kwamba utaanguka; kutakuwa mvua ya kufurika; nanyi, enyi mvua ya mawe makubwa ya barafu, mtaanguka; na upepo wa dhoruba utaupasua. Na huo ukuta utakapoanguka, je! Hamtaambiwa, Kuko wapi kupaka kwenu mlikoupaka? Basi Bwana MUNGU asema hivi; Nitaupasua kwa upepo wa dhoruba, katika ghadhabu yangu; tena kutakuwa mvua ya barafu ya kufurika katika hasira yangu; na mawe makubwa ya barafu katika hasira ya kuukomesha. Ndivyo nitakavyoubomoa ukuta mlioupaka chokaa isiyokorogwa vema, na kuuangusha chini, hata misingi yake itafunuliwa; nao utaanguka, nanyi mtaangamizwa katikati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu juu ya ukuta ule, na juu yao walioupaka chokaa isiyokorogwa vema; nami nitawaambieni, Ukuta huo hauko sasa, wala wao walioupaka hawako; yaani, manabii wa Israeli, watabirio habari za Yerusalemu, na kuona maono ya amani katika habari zake; wala hapana amani, asema Bwana MUNGU.