Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 29:10-28

Kutoka 29:10-28 BHN

“Kisha utamleta yule ndama dume mbele ya hema la mkutano. Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha ndama huyo na kumchinja mbele ya Mwenyezi-Mungu, mlangoni pa hema la mkutano. Utachukua kiasi cha damu na kuipaka kwenye pembe za madhabahu kwa kidole chako, na damu yote inayosalia utaimwaga chini ya madhabahu. Halafu utatwaa mafuta yote yanayofunika matumbo, sehemu bora ya maini pamoja na figo mbili na mafuta yake, uviteketeze vyote juu ya madhabahu. Lakini nyama ya fahali huyo pamoja na ngozi na mavi yake utavichukua na kuviteketeza nje ya kambi yenu. Hii itakuwa sadaka ya kuondoa dhambi. “Kisha utamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumwambia Aroni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake. Nawe utamchinja na damu yake utairashia madhabahu pande zake zote. Halafu utamkata huyo kondoo vipandevipande; utaosha matumbo yake na miguu yake, uviweke vyote pamoja na kichwa na vipande vingine. Kisha utamteketeza kondoo mzima juu ya madhabahu ili kunitolea sadaka ya kuteketezwa; harufu ya sadaka inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. “Utamchukua yule kondoo mwingine, naye Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. Nawe utamchinja na kuchukua kiasi cha damu na kumpaka Aroni na wanawe kwenye ncha za masikio yao ya kulia na vidole gumba vya mikono yao ya kulia, na vidole gumba vya miguu yao ya kulia. Damu inayobaki utairashia madhabahu pande zake zote. Kisha utachukua kiasi cha damu iliyoko juu ya madhabahu pamoja na yale mafuta ya kupaka umnyunyizie Aroni na mavazi yake, uwanyunyizie pia wanawe na mavazi yao. Aroni na wanawe watakuwa wamewekwa wakfu kwangu pamoja na mavazi yao yote. “Kisha utachukua mafuta ya huyo kondoo dume: Mkia wake, mafuta yanayofunika matumbo na sehemu bora ya maini, figo zake mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Kondoo huyo ni kondoo wa kuweka wakfu.) Kutoka katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu kilicho mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu, utachukua mkate mmoja na andazi moja lililotiwa mafuta na mkate mwembamba mmoja. Vyote hivi utamkabidhi Aroni na wanawe nao wataviinua juu kuwa ishara ya kunitolea tambiko mimi Mwenyezi-Mungu. Kisha utavichukua tena kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu pamoja na ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri itakayonipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. Hiyo ni sadaka inayotolewa kwa moto. “Kisha utachukua kidari cha huyo kondoo wa kumweka wakfu Aroni, na kufanya ishara ya kunitolea mimi Mwenyezi-Mungu. Nacho kitakuwa sehemu yako. Kuhani anapowekwa wakfu, kidari na paja la kondoo dume wa kuwekea wakfu vitaletwa na kuwekwa wakfu mbele yangu kwa kufanya ishara ya kunitolea, navyo vitakuwa vya Aroni na wanawe. Hivyo Waisraeli daima watachukua sehemu hizo kutoka katika sadaka zao za amani wanazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu na kumpa Aroni na wanawe. Hiyo ni sadaka yao kwa Mwenyezi-Mungu.

Soma Kutoka 29