Kutoka 29:10-28
Kutoka 29:10-28 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kisha utamleta yule ndama dume mbele ya hema la mkutano. Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha ndama huyo na kumchinja mbele ya Mwenyezi-Mungu, mlangoni pa hema la mkutano. Utachukua kiasi cha damu na kuipaka kwenye pembe za madhabahu kwa kidole chako, na damu yote inayosalia utaimwaga chini ya madhabahu. Halafu utatwaa mafuta yote yanayofunika matumbo, sehemu bora ya maini pamoja na figo mbili na mafuta yake, uviteketeze vyote juu ya madhabahu. Lakini nyama ya fahali huyo pamoja na ngozi na mavi yake utavichukua na kuviteketeza nje ya kambi yenu. Hii itakuwa sadaka ya kuondoa dhambi. “Kisha utamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumwambia Aroni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake. Nawe utamchinja na damu yake utairashia madhabahu pande zake zote. Halafu utamkata huyo kondoo vipandevipande; utaosha matumbo yake na miguu yake, uviweke vyote pamoja na kichwa na vipande vingine. Kisha utamteketeza kondoo mzima juu ya madhabahu ili kunitolea sadaka ya kuteketezwa; harufu ya sadaka inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. “Utamchukua yule kondoo mwingine, naye Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. Nawe utamchinja na kuchukua kiasi cha damu na kumpaka Aroni na wanawe kwenye ncha za masikio yao ya kulia na vidole gumba vya mikono yao ya kulia, na vidole gumba vya miguu yao ya kulia. Damu inayobaki utairashia madhabahu pande zake zote. Kisha utachukua kiasi cha damu iliyoko juu ya madhabahu pamoja na yale mafuta ya kupaka umnyunyizie Aroni na mavazi yake, uwanyunyizie pia wanawe na mavazi yao. Aroni na wanawe watakuwa wamewekwa wakfu kwangu pamoja na mavazi yao yote. “Kisha utachukua mafuta ya huyo kondoo dume: Mkia wake, mafuta yanayofunika matumbo na sehemu bora ya maini, figo zake mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Kondoo huyo ni kondoo wa kuweka wakfu.) Kutoka katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu kilicho mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu, utachukua mkate mmoja na andazi moja lililotiwa mafuta na mkate mwembamba mmoja. Vyote hivi utamkabidhi Aroni na wanawe nao wataviinua juu kuwa ishara ya kunitolea tambiko mimi Mwenyezi-Mungu. Kisha utavichukua tena kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu pamoja na ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri itakayonipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. Hiyo ni sadaka inayotolewa kwa moto. “Kisha utachukua kidari cha huyo kondoo wa kumweka wakfu Aroni, na kufanya ishara ya kunitolea mimi Mwenyezi-Mungu. Nacho kitakuwa sehemu yako. Kuhani anapowekwa wakfu, kidari na paja la kondoo dume wa kuwekea wakfu vitaletwa na kuwekwa wakfu mbele yangu kwa kufanya ishara ya kunitolea, navyo vitakuwa vya Aroni na wanawe. Hivyo Waisraeli daima watachukua sehemu hizo kutoka katika sadaka zao za amani wanazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu na kumpa Aroni na wanawe. Hiyo ni sadaka yao kwa Mwenyezi-Mungu.
Kutoka 29:10-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha utamleta huyo ng'ombe mbele ya hema ya kukutania; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo ng'ombe. Kisha utamchinja huyo ng'ombe mbele ya BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania. Kisha twaa baadhi ya damu ya ng'ombe, uitie katika pembe za madhabahu kwa kidole chako; na kuimimina damu yote chini ya madhabahu. Kisha twaa mafuta yote yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo juu yake, uyateketeze yote juu ya madhabahu. Lakini nyama yake huyo ng'ombe, na ngozi yake, na mavi yake, utayachoma kwa moto nje ya kambi; ni sadaka kwa ajili ya dhambi. Pia mtwae kondoo dume mmoja; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo dume. Kisha utamchinja huyo kondoo dume, na kuitwaa damu yake, na kuinyunyiza katika madhabahu kuizunguka kandokando. Kisha utamkatakata kondoo vipande vyake, na kuyaosha matumbo yake na miguu yake, na kuiweka pamoja na vipande vyake na kichwa chake. Nawe mteketeze kondoo mzima juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya BWANA; ni harufu nzuri, sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Kisha mtwae huyo kondoo wa pili; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo. Kisha utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la Haruni la upande wa kulia, na katika ncha za masikio ya kulia ya wanawe, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kulia, na katika vidole vikuu vya miguu yao ya kulia, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka kandokando. Kisha twaa katika hiyo damu iliyo juu ya madhabahu, na katika hayo mafuta ya kutiwa, na kumnyunyizia Haruni, juu ya mavazi yake, na wanawe, na mavazi yao pia, pamoja naye; naye atatakaswa, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye. Tena yatwae mafuta ya huyo kondoo dume, na mkia wake wa mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo katika hizo figo, na paja la kulia; kwani ni kondoo ambaye ni wa kuwekwa kwa kazi takatifu; utwae na mkate mmoja wa unga, na mkate mmoja ulioandaliwakwa mafuta, na kaki moja katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichowekwa mbele ya BWANA; nawe utavitia hivi vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe; nawe utavitikisatikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA. Kisha uvitwae vile vitu mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri mbele ya BWANA; ni sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Kisha twaa kidari cha huyo kondoo wa kuwekwa kwake Haruni kwa kazi takatifu, na kukitikisatikisa kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; nacho kitakuwa ni sehemu yako. Nawe kitakase kile kidari cha ile sadaka ya kutikiswa, na lile paja la sadaka ya kuinuliwa, lililotikiswa, na lililoinuliwa juu, vya yule kondoo wa kuwekwa kwa kazi takatifu, huyo aliyekuwa kwa ajili ya Haruni, na huyo aliyekuwa kwa ajili ya wanawe; navyo vitakuwa vya Haruni na wanawe posho ya lazima sikuzote itokayo kwa hao wana wa Israeli; kwa kuwa ni sadaka ya kuinuliwa; nayo itakuwa ni sadaka ya kuinuliwa itokayo kwa hao wana wa Israeli katika dhabihu zao za sadaka za amani, ni sadaka yao ya kuinuliwa kwa ajili ya BWANA.
Kutoka 29:10-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha utamleta huyo ng’ombe mbele ya hema ya kukutania; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo ng’ombe. Kisha utamchinja huyo ng’ombe mbele ya BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania. Kisha twaa baadhi ya damu ya ng’ombe, uitie katika pembe za madhabahu kwa kidole chako; na kuimimina damu yote chini ya madhabahu. Kisha twaa mafuta yote yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo juu yake, uyateketeze yote juu ya madhabahu. Lakini nyama yake huyo ng’ombe, na ngozi yake, na mavi yake, utayachoma kwa moto nje ya marago; ni sadaka kwa ajili ya dhambi. Pia mtwae kondoo mume mmoja; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo mume. Kisha utamchinja huyo kondoo mume, na kuitwaa damu yake, na kuinyunyiza katika madhabahu kuizunguka kando-kando. Kisha utamkata-kata kondoo vipande vyake, na kuyaosha matumbo yake na miguu yake, na kuiweka pamoja na vipande vyake na kichwa chake. Nawe mteketeze kondoo mzima juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya BWANA; ni harufu nzuri, sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Kisha mtwae huyo kondoo wa pili; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo. Kisha utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la Haruni la upande wa kuume, na katika ncha za masikio ya kuume ya wanawe, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vikuu vya miguu yao ya kuume, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka kando-kando. Kisha twaa katika hiyo damu iliyo juu ya madhabahu, na katika hayo mafuta ya kutiwa, na kumnyunyizia Haruni, juu ya mavazi yake, na wanawe, na mavazi yao pia, pamoja naye; naye atatakaswa, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye. Tena yatwae mafuta ya huyo kondoo mume, na mkia wake wa mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo katika hizo figo, na paja la kuume; kwani ni kondoo ambaye ni wa kuwekwa kwa kazi takatifu; utwae na mkate mmoja wa unga, na mkate mmoja ulioandaliwa kwa mafuta, na kaki moja katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichowekwa mbele ya BWANA; nawe utavitia hivi vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe; nawe utavitikisa-tikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA. Kisha uvitwae vile vitu mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri mbele ya BWANA; ni sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Kisha twaa kidari cha huyo kondoo wa kuwekwa kwake Haruni kwa kazi takatifu, na kukitikisa-tikisa kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; nacho kitakuwa ni sehemu yako. Nawe kitakase kile kidari cha ile sadaka ya kutikiswa, na lile paja la sadaka ya kuinuliwa, lililotikiswa, na lililoinuliwa juu, vya yule kondoo wa kuwekwa kwa kazi takatifu, huyo aliyekuwa kwa ajili ya Haruni, na huyo aliyekuwa kwa ajili ya wanawe; navyo vitakuwa vya Haruni na wanawe posho ya lazima sikuzote itokayo kwa hao wana wa Israeli; kwa kuwa ni sadaka ya kuinuliwa; nayo itakuwa ni sadaka ya kuinuliwa itokayo kwa hao wana wa Israeli katika dhabihu zao za sadaka za amani, ni sadaka yao ya kuinuliwa kwa ajili ya BWANA.
Kutoka 29:10-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Mlete yule fahali mbele ya Hema la Kukutania, naye Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. Mchinje huyo fahali mbele za BWANA kwenye mlango wa Hema la Kukutania. Chukua sehemu ya damu ya huyo fahali na kuipaka kwenye pembe za hayo madhabahu kwa kidole chako, na damu iliyobaki uimwage sehemu ya chini ya madhabahu. Kisha chukua mafuta yote ya huyo mnyama ya sehemu za ndani, yale yanayofunika ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake, uviteketeze juu ya madhabahu. Lakini nyama ya huyo fahali na ngozi yake na matumbo yake utavichoma nje ya kambi. Hii ni sadaka ya dhambi. “Chukua mmoja wa wale kondoo dume, naye Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. Mchinje huyo kondoo dume, chukua damu yake na uinyunyize pande zote za hayo madhabahu. Mkate huyo kondoo dume vipande vipande na usafishe sehemu za ndani pamoja na miguu, ukiviweka pamoja na kichwa na vipande vingine. Kisha mteketeze huyo kondoo dume mzima juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA, harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto. “Mchukue yule kondoo dume mwingine, naye Aroni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake. Mchinje, uchukue sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye masikio ya Aroni na wanawe, kwenye vidole gumba vya mikono yao ya kuume, pia kwenye vidole gumba vya miguu yao ya kuume. Kisha nyunyiza hiyo damu pande zote za madhabahu. Pia chukua sehemu ya damu iliyo juu ya madhabahu na sehemu ya mafuta ya upako, umnyunyizie Aroni na mavazi yake, pia wanawe na mavazi yao. Ndipo Aroni na wanawe pamoja na mavazi yao watakuwa wamewekwa wakfu. “Chukua mafuta ya huyu kondoo dume, mafuta ya mkia, mafuta ya sehemu za ndani yale yanayofunika ini, figo zote mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Huyo ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu.) Kutoka kwenye kile kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichoko mbele za BWANA, chukua mkate, andazi lililokandwa kwa mafuta na mkate mdogo mwembamba. Viweke vitu hivi vyote mikononi mwa Aroni na wanawe na uviinue mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa. Kisha vichukue vitu hivyo kutoka mikononi mwao, uviteketeze juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kupendeza kwa BWANA, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto. Baada ya kuchukua kidari cha huyo kondoo dume wa kuwekwa wakfu kwa Aroni, kiinue mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa, nayo itakuwa fungu lako. “Weka wakfu zile sehemu za kondoo dume aliyetumika kwa kumweka wakfu Aroni na wanawe: kidari kile kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa. Siku zote hili litakuwa fungu la kawaida kutoka kwa Waisraeli kwa ajili ya Aroni na wanawe. Hili ni toleo la Waisraeli watakalotoa kwa BWANA kutoka sadaka zao za amani.