Waefeso 3:12-21
Waefeso 3:12-21 BHN
Basi, kwa kuungana na Kristo na kwa imani kwake, sisi tunathubutu kumwendea Mungu kwa matumaini. Kwa hiyo, nawaombeni msife moyo kwa sababu ya mateso ninayopata kwa ajili yenu, maana hayo ni kwa ajili ya utukufu wenu. Kwa sababu hiyo, nampigia magoti Baba, aliye asili ya jamaa zote duniani na mbinguni. Namwomba Mungu, kadiri ya utajiri wa utukufu wake, awajalieni kwa uwezo wa Roho wake, nguvu ya kuwa imara ndani yenu, naye Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani. Namwomba mpate kuwa na mzizi na msingi katika mapendo kusudi muweze kufahamu pamoja na watu wote wa Mungu jinsi upendo wa Kristo ueneavyo kwa mapana na marefu, kwa kimo na kina. Naam, mpate kujua upendo wa Kristo upitao elimu yote, mjazwe kabisa utimilifu wote wa Mungu. Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria; kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele! Amina.