Waefeso 3:12-21
Waefeso 3:12-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini. Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu kwenu. Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.
Waefeso 3:12-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, kwa kuungana na Kristo na kwa imani kwake, sisi tunathubutu kumwendea Mungu kwa matumaini. Kwa hiyo, nawaombeni msife moyo kwa sababu ya mateso ninayopata kwa ajili yenu, maana hayo ni kwa ajili ya utukufu wenu. Kwa sababu hiyo, nampigia magoti Baba, aliye asili ya jamaa zote duniani na mbinguni. Namwomba Mungu, kadiri ya utajiri wa utukufu wake, awajalieni kwa uwezo wa Roho wake, nguvu ya kuwa imara ndani yenu, naye Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani. Namwomba mpate kuwa na mzizi na msingi katika mapendo kusudi muweze kufahamu pamoja na watu wote wa Mungu jinsi upendo wa Kristo ueneavyo kwa mapana na marefu, kwa kimo na kina. Naam, mpate kujua upendo wa Kristo upitao elimu yote, mjazwe kabisa utimilifu wote wa Mungu. Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria; kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele! Amina.
Waefeso 3:12-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini. Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu wenu. Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.
Waefeso 3:12-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndani yake na kwa njia ya imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri. Kwa hiyo, nawaomba msikate tamaa kwa sababu ya mateso yangu kwa ajili yenu, hayo ni utukufu wenu. Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu. Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu, yeye atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.