Mhubiri 10
10
1Nzi waliokufa husababisha marashi kunuka;
upumbavu kidogo hubatilisha hekima na heshima.
2Moyo wa mwenye hekima humwongoza kutenda yaliyo sawa;
lakini mtu mpumbavu moyo wake humpotosha.
3Hata apitapo njiani, mpumbavu hutambulikana hivyo,
humjulisha kila mtu kwamba yeye ni mpumbavu.
4Mtawala akikuwakia hasira, usijiuzulu;
makosa makubwa huweza kufutwa ukiwa mnyenyekevu.
5Kuna uovu niliogundua hapa duniani, uovu unaosababishwa na watawala: 6Kwamba wapumbavu wanapewa kazi za madaraka ya juu, na matajiri wanachukua nafasi za mwisho. 7Nimeona watumwa wanapanda farasi, na wakuu wanatembea kwa miguu kama watumwa.
8Mchimba shimo hutumbukia mwenyewe,
abomoaye ukuta huumwa na nyoka.
9Mchonga mawe huumizwa nayo,
mkata kuni hukabiliwa na hatari.
10Nguvu nyingi zaidi zahitajika
kwa mtumiaji shoka butu lisilonolewa,
lakini kutumia hekima humfanya mtu afanikiwe.#10:10 maana katika Kiebrania si dhahiri.
11Nyoka akiuma kabla hajachochewa,
mchochezi hahitajiki tena.
12Maneno ya mwenye hekima humnufaisha asemaye;
lakini midomo ya mpumbavu humwangamiza.
13Mpumbavu huanza kusema kwa maneno ya kijinga,
na kumaliza kauli yake kwa wazimu mbaya.
14Mpumbavu hububujika maneno.
Binadamu hajui yatakayokuwako,
wala yale yatakayotukia baada yake.
15Mpumbavu huchoshwa na kazi yake
hata asijue njia ya kurudia nyumbani.#10:15 labda kwa maana ya “hata vitu rahisi kama kwenda mjini hajui”: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
16Ole wako, ewe nchi, mtawala wako akiwa kijana,
na viongozi wako wakifanya sherehe asubuhi.
17Heri yako, ewe nchi, mtawala wako akiwa mtu wa heshima,
na viongozi wako wakifanya sherehe wakati wa kufaa,
ili kujipatia nguvu na si kujilewesha.
18Kutokana na uvivu wa mtu, paa hubonyea;
kwa sababu ya uzembe, nyumba huvuja.
19Chakula ni kwa ajili ya kujifurahisha,
divai huchangamsha maisha;
na fedha husababisha hayo yote.
20Usimwapize mtawala hata moyoni mwako,
wala usimwapize tajiri hata chumbani mwako unakolala,
kwa kuwa ndege ataisikia sauti yako,
au kiumbe arukaye atatangaza maneno yako.
Iliyochaguliwa sasa
Mhubiri 10: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.