Kumbukumbu la Sheria 5:1-17
Kumbukumbu la Sheria 5:1-17 BHN
Mose aliwaita pamoja Waisraeli, akawaambia: “Enyi Waisraeli, sikilizeni masharti na maagizo ambayo ninayatamka mbele yenu leo. Jifunzeni hayo na kuyatekeleza kwa uangalifu. Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alifanya agano nasi mlimani Horebu. Hakufanya agano hilo na wazee wetu tu, bali alifanya na sisi sote ambao tuko hai hivi leo. Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi ana kwa ana huko mlimani katikati ya moto. Wakati huo mimi nilisimama kati yenu na Mwenyezi-Mungu, nikawatangazieni yale aliyoyasema, kwa kuwa nyinyi mliogopa ule moto na hamkupanda mlimani. Mwenyezi-Mungu alisema hivi, “ ‘Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri, ambako ulikuwa mtumwa. “ ‘Usiwe na miungu mingine ila mimi. “ ‘Usijifanyie sanamu za miungu za kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. “ ‘Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu. Nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wale wanichukiao. Lakini nawafadhili maelfu ya wale wanipendao na kuzishika amri zangu. “ ‘Usilitaje bure jina langu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; maana mimi ni Mwenyezi-Mungu sitaacha kumwadhibu yeyote afanyaye hivyo. Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka wakfu, kama mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nilivyokuamuru. Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote, lakini siku ya saba ni siku ya Sabato ambayo imetengwa kwa ajili yangu. Siku hiyo wewe usifanye kazi yoyote, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika vilevile kama wewe. Usisahau kwamba wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, nami Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nikakutoa huko kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyoshwa; ndiyo maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako nimekuamuru kuiadhimisha siku ya Sabato. “ ‘Waheshimu baba yako na mama yako, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako nilivyokuamuru; fanya hivyo ili uishi siku nyingi na kufanikiwa katika nchi ambayo ninakupatia. “ ‘Usiue.