Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 5:1-17

Kumbukumbu la Sheria 5:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu ninenazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuangalia kuzitenda. BWANA, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu. BWANA hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani, sisi sote tuliopo hapa, tu hai. BWANA alisema nanyi uso kwa uso mlimani, toka kati ya moto; (nami wakati ule nalisimama kati ya BWANA na ninyi, ili kuwaonyesha neno la BWANA; maana, mliogopa kwa sababu ya ule moto, wala hamkupanda mlimani); naye akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure Jina la BWANA, Mungu wako; maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia, mtu alitajaye jina lake bure. Ishike siku ya Sabato uitakase, kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng’ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako ye yote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe. Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa BWANA, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato. Waheshimu baba yako na mama yako; kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako. Usiue.

Kumbukumbu la Sheria 5:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Mose aliwaita pamoja Waisraeli, akawaambia: “Enyi Waisraeli, sikilizeni masharti na maagizo ambayo ninayatamka mbele yenu leo. Jifunzeni hayo na kuyatekeleza kwa uangalifu. Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alifanya agano nasi mlimani Horebu. Hakufanya agano hilo na wazee wetu tu, bali alifanya na sisi sote ambao tuko hai hivi leo. Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi ana kwa ana huko mlimani katikati ya moto. Wakati huo mimi nilisimama kati yenu na Mwenyezi-Mungu, nikawatangazieni yale aliyoyasema, kwa kuwa nyinyi mliogopa ule moto na hamkupanda mlimani. Mwenyezi-Mungu alisema hivi, “ ‘Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri, ambako ulikuwa mtumwa. “ ‘Usiwe na miungu mingine ila mimi. “ ‘Usijifanyie sanamu za miungu za kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. “ ‘Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu. Nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wale wanichukiao. Lakini nawafadhili maelfu ya wale wanipendao na kuzishika amri zangu. “ ‘Usilitaje bure jina langu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; maana mimi ni Mwenyezi-Mungu sitaacha kumwadhibu yeyote afanyaye hivyo. Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka wakfu, kama mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nilivyokuamuru. Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote, lakini siku ya saba ni siku ya Sabato ambayo imetengwa kwa ajili yangu. Siku hiyo wewe usifanye kazi yoyote, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika vilevile kama wewe. Usisahau kwamba wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, nami Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nikakutoa huko kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyoshwa; ndiyo maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako nimekuamuru kuiadhimisha siku ya Sabato. “ ‘Waheshimu baba yako na mama yako, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako nilivyokuamuru; fanya hivyo ili uishi siku nyingi na kufanikiwa katika nchi ambayo ninakupatia. “ ‘Usiue.

Kumbukumbu la Sheria 5:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu nisemazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuzizingatia. BWANA, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu. BWANA hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani, sisi sote tuliopo hapa, tu hai. BWANA alisema nanyi uso kwa uso mlimani, kutoka kati ya moto; (nami wakati ule nikiwa nimesimama kati ya BWANA na ninyi, ili kuwaonesha neno la BWANA; maana, mliogopa kwa sababu ya ule moto, wala hamkupanda mlimani); naye akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure Jina la BWANA, Mungu wako; maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia, mtu alitajaye jina lake bure. Ishike siku ya Sabato uitakase, kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe. Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa BWANA, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato. Waheshimu baba yako na mama yako; kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako. Usiue.

Kumbukumbu la Sheria 5:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mose akawaita Israeli wote, akawaambia: Ee Israeli, sikilizeni amri na sheria ninazowatangazia leo. Jifunzeni, na mwe na hakika kuzifuata. BWANA Mungu wetu alifanya Agano nasi katika mlima wa Horebu. Si kwamba BWANA alifanya Agano na baba zetu, bali alifanya nasi, nasi sote ambao tuko hai hapa leo. BWANA alisema nanyi uso kwa uso kutoka moto juu ya mlima. (Wakati huo nilisimama kati ya BWANA na ninyi kuwatangazia neno la BWANA, kwa sababu mliogopa ule moto, nanyi hamkupanda mlimani.) Naye Mungu alisema: “Mimi ndimi BWANA Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. “Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni au duniani chini au ndani ya maji. Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, BWANA Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, lakini ninaonyesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la BWANA Mungu wako, kwa kuwa BWANA hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure. Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka takatifu, kama BWANA Mungu wako alivyokuagiza. Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote. Lakini siku ya Saba ni Sabato kwa BWANA, Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wa kiume au mtumishi wa kike, wala ngʼombe wako, punda wako au mnyama wako yeyote, wala mgeni aliyeko malangoni mwako, ili kwamba mtumishi wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika kama wewe. Kumbuka mlikuwa watumwa huko Misri, na BWANA Mungu wenu aliwatoa huko kwa mkono wenye nguvu na kwa mkono ulionyooshwa. Kwa hiyo BWANA Mungu wako amekuagiza kuiadhimisha siku ya Sabato. Waheshimu baba yako na mama yako, kama BWANA Mungu wako alivyokuagiza, ili siku zako zipate kuwa nyingi na kufanikiwa katika nchi BWANA Mungu wako anayokupa. Usiue.