Kumbukumbu 5:1-17
Kumbukumbu 5:1-17 NEN
Mose akawaita Israeli wote, akawaambia: Ee Israeli, sikilizeni amri na sheria ninazowatangazia leo. Jifunzeni, na mwe na hakika kuzifuata. BWANA Mungu wetu alifanya Agano nasi katika mlima wa Horebu. Si kwamba BWANA alifanya Agano na baba zetu, bali alifanya nasi, nasi sote ambao tuko hai hapa leo. BWANA alisema nanyi uso kwa uso kutoka moto juu ya mlima. (Wakati huo nilisimama kati ya BWANA na ninyi kuwatangazia neno la BWANA, kwa sababu mliogopa ule moto, nanyi hamkupanda mlimani.) Naye Mungu alisema: “Mimi ndimi BWANA Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. “Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni au duniani chini au ndani ya maji. Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, BWANA Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, lakini ninaonyesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la BWANA Mungu wako, kwa kuwa BWANA hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure. Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka takatifu, kama BWANA Mungu wako alivyokuagiza. Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote. Lakini siku ya Saba ni Sabato kwa BWANA, Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wa kiume au mtumishi wa kike, wala ngʼombe wako, punda wako au mnyama wako yeyote, wala mgeni aliyeko malangoni mwako, ili kwamba mtumishi wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika kama wewe. Kumbuka mlikuwa watumwa huko Misri, na BWANA Mungu wenu aliwatoa huko kwa mkono wenye nguvu na kwa mkono ulionyooshwa. Kwa hiyo BWANA Mungu wako amekuagiza kuiadhimisha siku ya Sabato. Waheshimu baba yako na mama yako, kama BWANA Mungu wako alivyokuagiza, ili siku zako zipate kuwa nyingi na kufanikiwa katika nchi BWANA Mungu wako anayokupa. Usiue.