Kumbukumbu la Sheria 17:8-13
Kumbukumbu la Sheria 17:8-13 BHN
Inawezekana kukatokea mashtaka mengine yaliyo magumu mijini mwenu, kama vile kesi zihusuzo: Unajisi, mambo ya haki za watu, na madhara ya mwili. Ikitokea hivyo, mtaondoka na kwenda mahali alipopachagua Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na huko mtawaendea makuhani Walawi, na mwamuzi aliye kazini wakati huo, nanyi mtatoa mashtaka mbele yao, nao watatoa uamuzi wao. Kisha mtafanya kama watakavyowatangazieni pale mahali Bwana atakapopachagua; mtakuwa waangalifu kufanya yote kama watakavyowaagiza. Itawabidi kufanya kufuatana na maongozi watakayowapatia na uamuzi watakaoutoa kwenu. Msiache kutimiza kwa dhati hukumu watakayowatangazia. Naye mtu asiyejali kumtii kuhani au mwamuzi aliyewekwa hapo kumhudumia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, au mwamuzi, mtu huyo atauawa. Ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu. Watu wote watasikia na kuogopa wasifanye tena kitu kwa kutojali.