Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 28:11-31

Matendo 28:11-31 BHN

Baada ya miezi mitatu tulianza tena safari yetu kwa meli moja ya Aleksandria iitwayo “Miungu Pacha”. Meli hiyo ilikuwa imetia nanga kisiwani wakati wote wa baridi. Tulifika katika mji wa Sirakusa, tukakaa hapo kwa siku tatu. Toka huko tulingoa nanga, tukazunguka na kufika Regio. Baada ya siku moja, upepo ulianza kuvuma kutoka kusini, na baada ya siku mbili tulifika bandari ya Potioli. Huko tuliwakuta ndugu kadhaa ambao walituomba tukae nao kwa juma moja. Hivi ndivyo tulivyopata kufika Roma. Ndugu wa kule Roma walipopata habari zetu, wakaja kutulaki kwenye soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akapata moyo. Tulipofika Roma, Paulo aliruhusiwa kukaa peke yake pamoja na askari mmoja wa kumlinda. Baada ya siku tatu, Paulo aliwaita pamoja viongozi wa Kiyahudi wa mahali hapo. Walipokusanyika, Paulo aliwaambia, “Wananchi wenzangu, mimi, ingawa sikufanya chochote kibaya wala kupinga desturi za wazee wetu, nilitiwa nguvuni kule Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa Waroma. Waliponihoji na kuona kwamba sikuwa na hatia yoyote, walitaka kuniachia. Lakini Wayahudi wengine walipinga jambo hilo, nami nikalazimika kukata rufani kwa Kaisari, ingawa sikuwa na chochote cha kuwashtaki wananchi wenzangu. Ni kwa sababu hiyo nimeomba kuonana na kuongea nanyi, maana nimefungwa minyororo hii kwa sababu ya tumaini lile la Israeli.” Wao wakamwambia, “Sisi hatujapokea barua yoyote kutoka Yudea, wala hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa na kutoa habari rasmi au kusema chochote kibaya juu yako. Lakini tunafikiri inafaa tusikie kutoka kwako mwenyewe mambo yaliyo kichwani mwako. Kwa maana tujualo sisi kuhusu hicho kikundi ni kwamba kinapingwa kila mahali.” Basi, walipanga naye siku kamili ya kukutana, na wengi wakafika huko alikokuwa anakaa. Tangu asubuhi mpaka jioni Paulo aliwaeleza na kuwafafanulia juu ya ufalme wa Mungu, akijaribu kuwafanya wakubali habari juu ya Yesu kwa kutumia sheria na maandiko ya manabii. Baadhi yao walikubali maneno yake, lakini wengine hawakuamini. Basi, kukawa na mtengano wa fikira kati yao. Walipokuwa wanakwenda zao, Paulo alisema jambo hili: “Kweli ni sawa yale Roho Mtakatifu aliyowaarifu wazee wenu kwa njia ya nabii Isaya akisema: ‘Nenda kwa watu hawa ukawaambie: Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa; kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameziba masikio yao, wamefumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao. Wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.’” Halafu Paulo akasema, “Jueni basi, kwamba ujumbe wa Mungu juu ya wokovu umepelekwa kwa watu wa mataifa. Wao watasikiliza!” [ Paulo alipokwisha sema hayo, Wayahudi walijiondokea huku wakiwa wanabishana vikali wao kwa wao.] Kwa muda wa miaka miwili mizima Paulo aliishi katika nyumba aliyoipanga yeye mwenyewe; akawa anawakaribisha wote waliofika kumsalimu. Alikuwa akihubiri ufalme wa Mungu na kufundisha juu ya Bwana Yesu Kristo kwa uhodari, bila kizuizi.

Video for Matendo 28:11-31

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 28:11-31