Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mdo 28:11-31

Mdo 28:11-31 SUV

Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha. Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu. Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli. Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi. Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka. Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda. Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, hata walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu. Na hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yo yote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nalikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli. Wale wakamwambia, Sisi hatukupata nyaraka zenye habari zako kutoka Uyahudi, wala hapana ndugu hata mmoja aliyefika hapa na kutupasha habari, au kunena neno baya juu yako. Lakini tunataka kusikia kwako uonavyo wewe; kwa maana katika habari za madhehebu hiyo imejulikana kwetu kwamba inanenwa vibaya kila mahali. Wakiisha kuagana naye siku, wakamjia katika nyumba aliyokaa, watu wengi sana, akawaeleza kwa taratibu na kuushuhudia ufalme wa Mungu, akiwaonya mambo yake Yesu, kwa maneno ya sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hata jioni. Wengine waliamini yale yaliyonenwa, wengine hawakuyaamini. Na walipokuwa hawapatani wao kwa wao, wakaenda zao, Paulo alipokwisha kusema neno hili moja, ya kwamba, Roho Mtakatifu alinena vema na baba zetu, kwa kinywa cha nabii Isaya, akisema, Enenda kwa watu hawa, ukawaambie, Kusikia, mtasikia wala hamtafahamu; Na kuona, mtaona wala hamtatambua; Kwa maana mioyo ya watu hawa imepumbaa, Na masikio yao ni mazito ya kusikia, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Na kusikia kwa masikio yao, Na kufahamu kwa mioyo yao, Na kubadili nia zao, nikawaponya. Basi ijulikane kwenu ya kwamba wokovu huu wa Mungu umepelekwa kwa Mataifa, nao watasikia! [ Alipokwisha kusema hayo, Wayahudi wakaenda zao, wakiulizana mengi wao kwa wao.] Akakaa muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.

Soma Mdo 28

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mdo 28:11-31

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha