Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 17:1-12

Matendo 17:1-12 BHN

Kwa kupitia Amfipoli na Apolonia, walisafiri mpaka Thesalonike ambako kulikuwa na sunagogi la Wayahudi. Paulo alijiunga nao kama ilivyokuwa desturi yake, akajadiliana nao Sabato tatu mfululizo, akitumia Maandiko Matakatifu. Aliyaeleza na kuonesha kwamba ilimbidi Kristo kuteswa na kufufuka kutoka kwa wafu. Akawaambia, “Yesu ambaye mimi namhubiri kwenu ndiye Kristo.” Baadhi yao walikubali wakajiunga na Paulo na Sila. Kadhalika, idadi kubwa ya Wagiriki waliomcha Mungu pamoja na wanawake wengi wa tabaka la juu, walijiunga nao. Lakini Wayahudi wakaona wivu; wakawakodi wafidhuli sokoni, wakafanya kikundi na kuzusha fujo mjini kote. Wakaivamia nyumba ya Yasoni wakitumaini kuwapata humo Paulo na Sila ili wawalete hadharani. Lakini hawakuwapata na hivyo walimburuta Yasoni pamoja na ndugu wengine mpaka kwa wakuu wa mji, wakapiga kelele: “Watu hawa wamekuwa wakivuruga dunia yote na sasa wako hapa mjini. Yasoni amewakaribisha nyumbani kwake. Wote wanafanya kinyume cha amri ya Kaisari wakisema eti: ‘Kuna mfalme mwingine aitwaye Yesu.’” Kwa maneno hayo waliwatia wasiwasi wakuu wa mji na kundi la watu. Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha wakawaacha waende zao. Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi. Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa Thesalonike. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila yalikuwa kweli. Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa tabaka la juu na wanaume pia.

Video ya Matendo 17:1-12