Matendo 17:1-12
Matendo 17:1-12 SRUV
Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi. Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimokuwa, akahojiana nao kwa maneno ya Maandiko sabato tatu, akiyafunua na kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba, Yesu huyu ninayewaambia ninyi habari zake ndiye Kristo. Wengine miongoni mwao wakaamini, wakafuatana na Paulo na Sila; na Wagiriki waliomcha Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache. Na Wayahudi wakaona wivu, wakajitwalia watu kadhaa miongoni mwa watu ovyo wasio na sifa njema, nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji; na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako, na Yasoni amewakaribisha; na hawa wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri za Kaisari, wakisema na kusema yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu. Wakafadhaisha ule mkutano na wakubwa wa mji walipoyasikia hayo. Nao walipokwisha kumtoza dhamana Yasoni na wenziwe wakawaacha waende zao. Mara hao ndugu wakawatuma Paulo na Sila usiku hadi Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa hamu kuu, wakayachunguza Maandiko kila siku, ili waone kama mambo hayo ndivyo yalivyo. Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, wakiwemo wanawake wa Kigiriki wenye cheo na wanaume.