2 Mambo ya Nyakati 20:5-13
2 Mambo ya Nyakati 20:5-13 BHN
Yehoshafati akasimama katikati ya kusanyiko la watu wa Yuda na Yerusalemu mbele ya ua mpya wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaomba kwa sauti akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zetu, wewe ndiwe Mungu uliye mbinguni! Wewe unazitawala falme zote duniani; unao uwezo na nguvu, wala hakuna awezaye kukupinga. Ni wewe ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii wakati watu wako Israeli walipoingia katika nchi hii, ukawapa wazawa wa Abrahamu rafiki yako, iwe yao milele. Nao wamekaa humu, na kukujengea hekalu kwa heshima ya jina lako, wakijua kwamba wakipatwa na maafa yoyote, vita, maradhi mabaya, au njaa, basi watakuja na kusimama mbele ya nyumba hii mbele yako, wakulilie katika shida zao, nawe utawasikiliza na kuwaokoa. Sasa watu wa Amoni, Moabu na wa mlima Seiri, ambao hukuwaruhusu babu zetu washambulie nchi zao walipotoka Misri, wakapitia kandokando wasiwaangamize, tazama, jinsi wanavyotulipa. Wanakuja kututoa katika nchi yako uliyotupa iwe mali yetu. Wewe ndiwe Mungu wetu! Waadhibu, kwani sisi hatuna uwezo wowote mbele ya jeshi kubwa kama hili linalotujia. Hatujui la kufanya ila tunatazamia msaada kutoka kwako.” Wanaume wote wa Yuda, pamoja na wake zao na watoto wao, walikuwa wamesimama hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu.