2 Nyakati 20:5-13
2 Nyakati 20:5-13 NENO
Kisha Yehoshafati akasimama katika kusanyiko la Yuda na Yerusalemu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, mbele ya ua mpya, akasema: “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zetu, si wewe ndiwe uliye Mungu mbinguni? Si wewe ndiwe unayetawala juu ya falme zote za mataifa? Uweza na nguvu viko mkononi mwako, wala hakuna yeyote anayeweza kushindana nawe. Je, si ni wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, na ukawapa wazao wa rafiki yako Ibrahimu hata milele? Wameishi ndani yake na humo wamekujengea mahali patakatifu kwa ajili ya Jina lako, wakisema: ‘Kama maafa yakitujia, ikiwa ni upanga, hukumu, tauni, au njaa, tutasimama mbele zako, mbele ya Hekalu hili ambalo limeitwa kwa Jina lako na kukulilia katika shida yetu, nawe utatusikia na kutuokoa.’ “Lakini sasa hawa watu wa Amoni, Moabu na Mlima Seiri, ambao hukuwaruhusu Israeli wazivamie nchi zao wakati walitoka Misri; hivyo wakageukia mbali nao na hawakuwaangamiza. Tazama jinsi wanavyotulipa kwa kuja kututupa nje ya milki uliyotupatia sisi kuwa urithi. Ee Mungu wetu, je, wewe hutawahukumu? Kwa kuwa sisi hatuna uwezo wa kukabiliana na jeshi hili kubwa linalokuja kutushambulia. Sisi hatujui la kufanya, bali macho yetu yanakutazama wewe.” Wanaume wote wa Yuda pamoja na wake zao, watoto wao na wadogo wao wakasimama pale mbele za Mwenyezi Mungu.