Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 29:1-11

1 Samueli 29:1-11 BHN

Wafilisti walikusanya majeshi yao yote huko Afeka, na Waisraeli walipiga kambi kwenye chemchemi ya bonde la Yezreeli. Wakuu watano wa Wafilisti walipokuwa wakipita na vikosi vyao vya mamia na maelfu, Daudi naye akiwa na watu wake pamoja na Akishi walikuwa wanafuata upande wa nyuma wa jeshi hilo. Makamanda wa Wafilisti waliuliza, “Waebrania hawa wanafanya nini hapa?” Akishi akawajibu hao makamanda Wafilisti, “Huyu ni Daudi, mtumishi wa Shauli mfalme wa Israeli; naye amekuwa nami kwa muda mrefu: Miaka kadhaa. Na tangu alipokimbilia kwangu, sijampata na kosa lolote.” Lakini makamanda wa Wafilisti walimkasirikia sana Akishi, wakamwambia, “Mrudishe aende mahali ulikompa akae. Kamwe asiende pamoja nasi vitani, la sivyo wakati wa vita atageuka na kuwa adui yetu. Huoni kuwa mtu huyu atapata njia nzuri ya kupatana na bwana wake halafu kuwa adui yetu vitani? Je, huyu si Daudi yuleyule ambaye wanawake waliimba habari zake walipokuwa wakicheza, ‘Shauli ameua maelfu, lakini Daudi ameua maelfu kumi.’” Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba umekuwa mwaminifu kwangu. Lingekuwa jambo jema kwangu twende wote vitani, kwa maana sijaona lolote baya kwako tangu siku ile ulipokuja kwangu hadi leo hii. Hata hivyo, wakuu hawajaridhika nawe. Hivyo sasa, rudi nyumbani. Nenda kwa amani ili usiwachukize wakuu wa Wafilisti.” Daudi akamwambia Akishi, “Lakini nimefanya nini? Kama unavyosema kuwa, hujaniona na kosa lolote tangu siku ile nilipoanza kukutumikia hadi leo, kwa nini nisiende kupigana na maadui za bwana wangu, mfalme?” Akishi akamwambia, “Najua kuwa huna lawama mbele yangu kama malaika wa Mungu. Hata hivyo, makamanda wa Wafilisti wamesema, ‘Kamwe asiende pamoja nasi vitani’. Sasa, wewe pamoja na watumishi wa bwana wako Shauli waliokuja pamoja nawe, kesho asubuhi na mapema, amkeni na kuondoka mara kunapopambazuka.” Hivyo, kesho yake asubuhi, Daudi pamoja na watu wake waliondoka kurudi katika nchi ya Wafilisti. Lakini hao Wafilisti wakaenda Yezreeli.