Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 29:1-11

1 Samueli 29:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Wafilisti walikusanya majeshi yao yote huko Afeka, na Waisraeli walipiga kambi kwenye chemchemi ya bonde la Yezreeli. Wakuu watano wa Wafilisti walipokuwa wakipita na vikosi vyao vya mamia na maelfu, Daudi naye akiwa na watu wake pamoja na Akishi walikuwa wanafuata upande wa nyuma wa jeshi hilo. Makamanda wa Wafilisti waliuliza, “Waebrania hawa wanafanya nini hapa?” Akishi akawajibu hao makamanda Wafilisti, “Huyu ni Daudi, mtumishi wa Shauli mfalme wa Israeli; naye amekuwa nami kwa muda mrefu: Miaka kadhaa. Na tangu alipokimbilia kwangu, sijampata na kosa lolote.” Lakini makamanda wa Wafilisti walimkasirikia sana Akishi, wakamwambia, “Mrudishe aende mahali ulikompa akae. Kamwe asiende pamoja nasi vitani, la sivyo wakati wa vita atageuka na kuwa adui yetu. Huoni kuwa mtu huyu atapata njia nzuri ya kupatana na bwana wake halafu kuwa adui yetu vitani? Je, huyu si Daudi yuleyule ambaye wanawake waliimba habari zake walipokuwa wakicheza, ‘Shauli ameua maelfu, lakini Daudi ameua maelfu kumi.’” Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba umekuwa mwaminifu kwangu. Lingekuwa jambo jema kwangu twende wote vitani, kwa maana sijaona lolote baya kwako tangu siku ile ulipokuja kwangu hadi leo hii. Hata hivyo, wakuu hawajaridhika nawe. Hivyo sasa, rudi nyumbani. Nenda kwa amani ili usiwachukize wakuu wa Wafilisti.” Daudi akamwambia Akishi, “Lakini nimefanya nini? Kama unavyosema kuwa, hujaniona na kosa lolote tangu siku ile nilipoanza kukutumikia hadi leo, kwa nini nisiende kupigana na maadui za bwana wangu, mfalme?” Akishi akamwambia, “Najua kuwa huna lawama mbele yangu kama malaika wa Mungu. Hata hivyo, makamanda wa Wafilisti wamesema, ‘Kamwe asiende pamoja nasi vitani’. Sasa, wewe pamoja na watumishi wa bwana wako Shauli waliokuja pamoja nawe, kesho asubuhi na mapema, amkeni na kuondoka mara kunapopambazuka.” Hivyo, kesho yake asubuhi, Daudi pamoja na watu wake waliondoka kurudi katika nchi ya Wafilisti. Lakini hao Wafilisti wakaenda Yezreeli.

1 Samueli 29:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki; nao Waisraeli wakafanya kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli. Nao wakuu wa Wafilisti wakapita mbele, mamia, na maelfu; naye Daudi na watu wake wakapita wa mwisho pamoja na Akishi. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakasema, Waebrania hawa wanafanya nini hapa? Naye Akishi akawaambia wakuu wa Wafilisti, Je! Siye huyu Daudi, yule mtumishi wa Sauli, mfalme wa Israeli, ambaye amefuatana na mimi siku hizi, naam, miaka hii, wala mimi nisione hatia kwake, tangu hapo aliponiangukia mimi hata leo? Lakini wakuu wa Wafilisti wakamkasirikia, na kumwambia, Mrudishe huyu, apate kurejea mahali pake ulipomwagiza, wala asiende pamoja nasi vitani, asije akawa adui wetu vitani; kwani mtu huyu angejipatanisha na bwana wake kwa njia gani? Je! Si kwa vichwa vya watu hawa? Je! Siye huyo Daudi, ambaye waliimbiana habari zake katika michezo, wakisema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake? Ndipo Akishi akamwita Daudi, akamwambia, Aishivyo BWANA, wewe umekuwa mwenye adili, tena kutoka kwako na kuingia kwako pamoja nami katika jeshi ni kwema machoni pangu; kwa sababu mimi sikuona uovu ndani yako tangu siku ile uliponijia hata leo; walakini hao wakuu hawakuridhii. Basi sasa rudi, uende zako kwa amani, ili usiwachukize hao wakuu wa Wafilisti. Naye Daudi akamwambia Akishi, Lakini mimi nimefanyaje? Nawe umeona nini kwangu mimi mtumishi wako, muda wote niliokaa mbele yako hata leo, nisipate ruhusa niende na kupigana na adui za bwana wangu mfalme? Akishi akajibu, akamwambia Daudi, Mimi najua ya kuwa u mwema machoni pangu, kama malaika wa Mungu; ila hao wakuu wa Wafilisti wamesema, Huyu hatakwea pamoja nasi kwenda vitani. Kwa hiyo sasa amka asubuhi na mapema, wewe na watumishi wa bwana wako waliokuja pamoja nawe; nanyi mtakapoamka asubuhi na mapema, na kupata mwanga, nendeni zenu. Basi Daudi akaamka asubuhi na mapema, yeye na watu wake, kwenda zao asubuhi, kuirudia nchi ya Wafilisti. Nao Wafilisti wakakwea kwenda Yezreeli.

1 Samueli 29:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki; nao Waisraeli wakafanya kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli. Nao mashehe wa Wafilisti wakapita mbele, mia kwa mia, na elfu kwa elfu; naye Daudi na watu wake wakapita wa mwisho pamoja na Akishi. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakasema, Waebrania hawa wafanyani hapa? Naye Akishi akawaambia wakuu wa Wafilisti, Je! Siye huyu Daudi, yule mtumishi wa Sauli, mfalme wa Israeli, ambaye amefuatana na mimi siku hizi, naam, miaka hii, wala mimi nisione hatia kwake, tangu hapo aliponiangukia mimi hata leo? Lakini wakuu wa Wafilisti wakamkasirikia; nao wakuu wa Wafilisti wakamwambia, Mrudishe huyu, apate kurejea mahali pake ulipomwagiza, wala asiende pamoja nasi vitani, asije akawa adui wetu vitani; kwani mtu huyu angejipatanisha na bwana wake kwa njia gani? Je! Si kwa vichwa vya watu hawa? Je! Siye huyo Daudi, ambaye waliimbiana habari zake katika michezo, wakisema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake? Ndipo Akishi akamwita Daudi, akamwambia, Aishivyo BWANA, wewe umekuwa mwenye adili, tena kutoka kwako na kuingia kwako pamoja nami katika jeshi ni kwema machoni pangu; kwa sababu mimi sikuona uovu ndani yako tangu siku ile uliponijia hata leo; walakini hao wakuu hawakuridhii. Basi sasa urudi, uende zako kwa amani, ili usiwachukize hao mashehe wa Wafilisti. Naye Daudi akamwambia Akishi, Lakini mimi nimefanyaje? Nawe umeona nini kwangu mimi mtumwa wako, muda wote niliokaa mbele yako hata leo, nisipate ruhusa niende na kupigana na adui za bwana wangu mfalme? Akishi akajibu, akamwambia Daudi, Mimi najua ya kuwa u mwema machoni pangu, kama malaika wa Mungu; ila hao wakuu wa Wafilisti wamesema, Huyu hatakwea pamoja nasi kwenda vitani. Kwa hiyo sasa amka asubuhi na mapema, wewe na watumwa wa bwana wako waliokuja pamoja nawe; nanyi mtakapoamka asubuhi na mapema, na kupata mwanga, nendeni zenu. Basi Daudi akaamka asubuhi na mapema, yeye na watu wake, kwenda zao asubuhi, kuirudia nchi ya Wafilisti. Nao Wafilisti wakakwea kwenda Yezreeli.

1 Samueli 29:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki, nao Waisraeli wakapiga kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli. Watawala wa Wafilisti walipokuwa wakipita pamoja na vikosi vyao vya mamia na vya maelfu, Daudi na watu wake walikuwa wakitembea huko nyuma pamoja na Akishi. Majemadari wa Wafilisti wakauliza, “Vipi kuhusu hawa Waebrania?” Akishi akajibu, “Huyu si Daudi, aliyekuwa afisa wa Sauli mfalme wa Israeli? Ameshakuwa pamoja nami kwa zaidi ya mwaka, naye tangu alipomwacha Sauli hadi sasa, sikuona kosa lolote kwake.” Lakini majemadari wa Wafilisti wakamkasirikia na kusema, “Mrudishe mtu huyu, apate kurudi mahali pale ulipompangia. Haimpasi kufuatana pamoja nasi vitani, asije akageuka, akawa kinyume chetu vitani. Ni kwa njia ipi bora zaidi angeweza kujipatia tena kibali kwa bwana wake, isipokuwa kwa vichwa vya watu wetu wenyewe? Je, huyu si ndiye Daudi walioimba kumhusu katika ngoma zao, wakisema: “ ‘Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake’?” Basi Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Kama vile BWANA aishivyo, wewe umekuwa mtu mwaminifu, nami ningependa utumike pamoja nami katika jeshi. Tangu siku ile uliyofika kwangu hadi sasa, sijaona kosa lolote kwako, lakini hao watawala hawakukubali. Rudi na uende kwa amani; usifanye chochote cha kuwakasirisha watawala wa Kifilisti.” Daudi akamuuliza Akishi, “Lakini mimi nimefanya nini? Je, umeona nini kibaya juu ya mtumishi wako tangu siku ile niliyokuja kwako hadi leo? Kwa nini nisirudi na kupigana na adui za bwana wangu mfalme?” Akishi akamjibu Daudi, “Mimi ninajua ya kuwa wewe umekuwa wa kupendeza machoni pangu kama vile malaika wa Mungu. Lakini hao majemadari wa Wafilisti wamesema, ‘Huyu haimpasi kwenda vitani pamoja nasi.’ Sasa amka mapema, pamoja na watumishi wa bwana wako waliofuatana nawe, nanyi ondokeni asubuhi mara kutakapopambazuka.” Hivyo Daudi na watu wake wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda zao kurudi katika nchi ya Wafilisti, nao Wafilisti wakapanda kwenda Yezreeli.