Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 23:14-29

1 Samueli 23:14-29 BHN

Basi, Daudi alibaki ngomeni jangwani, katika nchi ya milima ya mbuga za Zifu. Shauli alimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia Daudi mikononi mwa Shauli. Daudi alijua kuwa Shauli alitaka kuyaangamiza maisha yake. Daudi akawa katika mbuga za Zifu, huko Horeshi. Yonathani mwana wa Shauli alimfuata Daudi huko Horeshi akamtia moyo kwamba Mungu anamlinda. Yonathani alimwambia, “Usiogope, baba yangu Shauli hatakupata. Wewe utakuwa mfalme wa Israeli, mimi nitakuwa wa pili wako. Hata Shauli baba yangu anajua jambo hili.” Hao wote wawili, wakafanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu. Daudi akabaki mjini Horeshi na Yonathani akaenda zake nyumbani. Shauli alipokuwa bado huko Gibea, Wazifu wakamwendea na kumwambia, “Daudi anajificha katika nchi yetu kwenye ngome huko Horeshi, kwenye mlima Hakila, ulio upande wa kusini wa Yeshimoni. Sasa, mfalme, njoo ili utekeleze yaliyomo moyoni mwako, na kwa upande wetu, jukumu letu litakuwa kumtia Daudi mikononi mwako.” Shauli akawajibu, “Nyinyi kweli mnanionea huruma; Mwenyezi-Mungu na awabariki. Nendeni, mkahakikishe tena, mjue mahali anapojificha, na ni nani amemwona mahali hapo; maana nimeambiwa kwamba yeye ni mjanja sana. Chunguzeni kila upande mjue mahali anapojificha, kisha mniletee habari kamili. Halafu nitakwenda pamoja nanyi na ikiwa bado atakuwa yuko huko, basi, mimi nitamsaka miongoni mwa maelfu yote ya watu wa Yuda.” Basi, wakaondoka kwenda Zifu, wakimtangulia Shauli. Wakati huo, Daudi na watu wake walikuwa katika jangwa la Maoni, katika bonde la Araba kusini mwa Yeshimoni. Shauli na watu wake wakaanza kumtafuta Daudi. Lakini Daudi alipoambiwa habari hizo, alikwenda kujificha kwenye miamba, iliyoko katika mbuga za Maoni na kukaa huko. Shauli aliposikia habari hizo, alimfuatilia Daudi huko kwenye mbuga za Maoni. Shauli na watu wake walikuwa upande mmoja wa mlima, na Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima. Daudi alipokuwa anaharakisha kukimbia, Shauli naye alikuwa anamkaribia kumkamata Daudi. Hapo mtu mmoja akamwendea Shauli na kumwambia, “Njoo haraka; Wafilisti wanaishambulia nchi.” Hivyo, Shauli akaacha kumfuatilia Daudi, akaenda kupigana na Wafilisti. Ndio maana mahali hapo pakaitwa “Mwamba wa Matengano.” Daudi aliondoka mahali hapo, akaenda kuishi kwenye ngome ya mji wa Engedi.