1 Samweli 23:14-29
1 Samweli 23:14-29 SRUV
Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake. Daudi akaona ya kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika nyika ya Zifu, huko Horeshi. Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu. Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa makamu wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu. Na hao wawili wakafanya agano mbele za BWANA; Daudi naye akakaa huko Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani kwake. Ndipo wale Wazifi wakakwea kwa Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha kwetu ngomeni mwa Horeshi, kilimani pa Hakila upande wa kusini wa Yeshimoni? Basi sasa, Ee mfalme, ushuke, kama utakavyo nafsini mwako kushuka; na kazi yetu itakuwa kumtia mkononi mwa mfalme. Naye Sauli akasema, Na mbarikiwe ninyi na BWANA; kwa sababu mmenihurumia. Nendeni, nawasihi, mkazidi kupata hakika, mkajue na kuona mahali pake anapojificha, tena ni nani aliyemwona huko; maana nimeambiwa ya kwamba ana ujanja mwingi. Chunguzeni basi, mkayajue maficho yake yote anapojificha; kisha njoni kwangu, tena msikose, nami nitakwenda pamoja nanyi; tena itakuwa, akiwapo katika nchi, mimi nitamtafutatafuta katika maelfu yote ya Yuda. Nao wakaondoka, wakaenda Zifu kumtangulia Sauli; lakini Daudi na watu wake walikuwapo nyikani pa Maoni, katika Araba upande wa kusini mwa jangwa. Basi Sauli na watu wake wakaenda kumtafuta. Watu wakamwambia Daudi; basi kwa hiyo akashuka mpaka mwambani, akakaa nyikani pa Maoni. Naye Sauli alipopata habari, alimwinda Daudi nyikani pa Maoni. Sauli akaenda upande huu wa mlima, na Daudi na watu wake wakaenda upande huu wa mlima; naye Daudi akafanya haraka sana ili amtoroke Sauli; kwa sababu Sauli na watu wake walikuwa wakiwazingira Daudi na watu wake ili kuwakamata. Lakini akaja mjumbe kwa Sauli, kusema, Njoo upesi, kwa kuwa Wafilisti wameishambulia nchi. Basi Sauli akarudi kutoka kumwinda Daudi, akaenda kupigana na Wafilisti; kwa hiyo wakapaita mahali pale, Selahamalekothi. Naye Daudi akakwea kutoka huko, akakaa katika ngome ya Engedi.