Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 1:1-18

1 Samueli 1:1-18 BHN

Kulikuwa na mtu mmoja mjini Rama katika nchi ya milima ya Efraimu aitwaye Elkana wa kabila la Efraimu. Yeye alikuwa mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu. Elkana alikuwa na wake wawili, mmoja aliitwa Hana na wa pili Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Kila mwaka Elkana alisafiri kutoka Rama kwenda kuabudu na kumtambikia Mwenyezi-Mungu wa majeshi kule Shilo. Huko, watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu. Kila wakati Elkana alipotoa tambiko alimpa mkewe Penina fungu moja la nyama ya tambiko na fungu mojamoja kwa watoto wake wa kiume na wa kike. Lakini Elkana alimpa Hana fungu moja ingawa alikuwa anampenda sana, na Mwenyezi-Mungu hakuwa amemjalia watoto. Lakini Penina, mchokozi wa Hana, daima alikuwa akimkasirisha vikali na kumuudhi Hana kwa kuwa Mwenyezi-Mungu hakumjalia watoto. Mambo haya yaliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Penina alimkasirisha Hana hata ikawa Hana analia na kukataa kula chochote. Elkana, mumewe, kila mara alimwuliza, “Kwa nini unalia? Kwa nini hutaki kula? Kwa nini una huzuni moyoni mwako? Je, mimi si bora kwako kuliko watoto kumi wa kiume?” Siku moja, walipokuwa wamemaliza kula na kunywa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, Hana akasimama. Wakati huo, kuhani Eli alikuwa amekaa kwenye kiti karibu na mwimo wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hana alikuwa na huzuni sana. Na alipokuwa anamwomba Mwenyezi-Mungu akawa analia kwa uchungu. Akaweka nadhiri akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kama tu utayaangalia mateso yangu mimi mtumishi wako ukanikumbuka mimi, bila kunisahau, mimi mtumishi wako, ukanijalia mimi mtumishi wako, mtoto wa kiume, nitakupa wewe Mwenyezi-Mungu mtoto huyo awe wako maisha yake yote; wembe hautapita kichwani pake kamwe.” Hana aliendelea kumwomba Mwenyezi-Mungu kwa muda mrefu, na kuhani Eli akawa anaangalia midomo yake. Hana alikuwa akiomba kimoyomoyo, lakini midomo yake ilikuwa inachezacheza, ila sauti yake haikusikika. Hivyo Eli akafikiri kuwa Hana amelewa. Kwa hiyo Eli akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achana na kunywa divai.” Lakini Hana akamjibu, “Sivyo bwana wangu; mimi ni mwanamke mwenye taabu mno; mimi sijanywa divai wala kinywaji kikali, bali nimekuwa nikimtolea Mwenyezi-Mungu yaliyomo rohoni mwangu. Usinidhanie kuwa mimi ni mwanamke asiyefaa kitu. Kwa muda wote huu nimekuwa nikisema mahangaiko yangu na taabu yangu.” Ndipo Eli akamwambia, “Nenda kwa amani; naye Mungu wa Israeli akupe kile ulichomwomba.” Hana akasema, “Naomba nami mtumishi wako nipate kibali mbele yako.” Hana akaenda zake, akala chakula na hakuwa na huzuni tena.