Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 1:1-18

1 Samweli 1:1-18 NEN

Kulikuwepo na mtu mmoja kutoka Rama, Msufi kutoka nchi ya vilima vya Efraimu, ambaye jina lake aliitwa Elikana mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu. Alikuwa na wake wawili, mmoja aliitwa Hana na mwingine Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na mtoto. Kila mwaka mtu huyu alikwea kutoka mji wake ili kuabudu na kutoa dhabihu kwa BWANA Mwenye Nguvu Zote huko Shilo, ambapo Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwa makuhani wa BWANA. Kila mara ilipofika siku ya Elikana kutoa dhabihu, aliwapa mafungu Penina mkewe na wanawe wote pamoja na binti zake. Lakini alimpa Hana fungu maradufu kwa sababu alimpenda, ingawa BWANA alikuwa amemfunga tumbo. Kwa sababu BWANA alikuwa amemfunga tumbo, mke mwenzake alikuwa anamchokoza ili kumuudhi. Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda katika nyumba ya BWANA, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha mpaka analia na kushindwa kula. Elikana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?” Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu la BWANA. Kwa uchungu wa rohoni Hana alilia sana na akamwomba BWANA. Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa BWANA kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.” Alipokuwa anaendelea kumwomba BWANA, Eli alichunguza kinywa chake. Hana alikuwa akiomba moyoni mwake, midomo yake ikiwa inachezacheza lakini sauti haikusikika. Eli akafikiri alikuwa amelewa naye akamwambia, “Utaendelea kulewa mpaka lini? Achilia mbali mvinyo wako.” Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwa BWANA. Usimdhanie mtumishi wako kuwa mwanamke mwovu; nimekuwa nikiomba hapa katika wingi wa uchungu mkuu na huzuni.” Eli akamjibu, “Nenda kwa amani, naye Mungu wa Israeli na akujalie kile ulichomwomba.” Hana akasema, “Mtumishi wako na apate kibali machoni pako.” Kisha akaondoka zake na kula chakula, wala uso wake haukuwa na huzuni tena.