1 Petro 5:6-14
1 Petro 5:6-14 BHN
Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa enzi wa Mungu, ili awainue wakati ufaao. Mwekeeni matatizo yenu yote, maana yeye anawatunzeni. Muwe macho; kesheni! Maana adui yenu, Ibilisi, huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mawindo. Muwe imara katika imani na kumpinga, mkijua kwamba ndugu zenu pote duniani wanapatwa na mateso hayohayo. Lakini mkisha teseka muda mfupi, Mungu aliye asili ya neema yote na ambaye anawaiteni kuushiriki utukufu wake wa milele katika kuungana na Kristo, yeye mwenyewe atawakamilisheni na kuwapeni uthabiti, nguvu na msingi imara. Kwake yawe mamlaka milele! Amina. Nimewaandikieni barua hii fupi kwa msaada wa Silwano, ndugu ambaye namjua na kumwamini. Nataka kuwapeni moyo na kushuhudia kwamba jambo hili ni neema ya Mungu kweli. Kaeni imara katika neema hiyo. Jumuiya ya wenzenu walioteuliwa na Mungu hapa Babuloni wanawasalimuni. Vilevile mwanangu Marko anawasalimuni. Salimianeni kwa ishara ya upendo wa Kikristo. Nawatakieni amani nyinyi mlio wake Kristo.