1 Petro 5:6-14
1 Petro 5:6-14 SRUV
Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. Muwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu kote duniani. Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawaimarisha, atawathibitisha, atawatia nguvu na kuwapa msingi imara. Uweza una yeye hata milele na milele. Amina. Kwa mkono wa Silwano, ndugu mwaminifu kama nijuavyo, nimewaandikia kwa maneno machache, kuonya na kushuhudia ya kuwa hii ndiyo neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika hiyo. Mwenzenu mteule hapa Babeli awasalimu, na Marko mwanangu. Salimianeni kwa busu la upendo. Amani na iwe kwenu nyote, mlio katika Kristo. Amina.