Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Petro 2:11-24

1 Petro 2:11-24 BHN

Wapenzi wangu, nawasihi nyinyi kama wageni na wakimbizi hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho. Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu siku ya kuja kwake. Basi, jiwekeni chini ya mamlaka yote ya kibinadamu, kwa ajili ya Bwana: Utii kwa mfalme aliye mtawala mkuu, utii kwa wakuu wa mikoa ambao wameteuliwa naye kuwaadhibu wahalifu na kuwasifu watendao mema. Maana Mungu anataka muweze kuyakomesha maneno ya kijinga ya watu wasio na akili kwa matendo mema mnayofanya. Ishini kama watu huru; lakini msiutumie uhuru wenu kuuficha ubaya, bali ishini kama watumishi wa Mungu. Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu zenu waamini, mcheni Mungu, mheshimuni mfalme. Enyi watumishi wa nyumbani, watiini wakuu wenu kwa heshima yote, wawe wema na wapole au wenye kuchukiza. Maana kama mnavumilia maumivu ya mateso msiyostahili kwa sababu mwajua kwamba Mungu anataka hivyo, basi Mungu atawafadhili. Maana, mtapata tuzo gani mkivumilia mapigo mnayostahili kwa sababu ya makosa yenu? Lakini kama mnavumilia mateso hata ingawa mmetenda mema, Mungu atawapeni baraka kwa ajili hiyo. Hayo ndiyo mliyoitiwa; maana Kristo mwenyewe aliteseka kwa ajili yenu, akawaachieni mfano, ili mfuate mwenendo wake. Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake. Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki. Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya msalaba, tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa majeraha yake, nyinyi mmeponywa.