1 Petro 2:11-24
1 Petro 2:11-24 NEN
Wapenzi, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu. Kwa ajili ya Bwana, tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu: Kwa mfalme kwani ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi, au kwa maafisa aliowaweka, kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale watendao mema. Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema mnyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu. Ishini kama watu huru, lakini msitumie uhuru wenu kama kisingizio cha kutenda uovu, bali ishini kama watumishi wa Mungu. Mheshimuni kila mtu ipasavyo: Wapendeni jamaa ya ndugu waumini, mcheni Mungu, mpeni heshima mfalme. Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu kwa heshima yote, si wale mabwana walio wema na wapole peke yao, bali pia wale walio wakali. Kwa maana ni jambo la sifa kama mtu akivumilia anapoteswa kwa uonevu kwa ajili ya Mungu. Kwani ni faida gani kwa mtu kustahimili anapopigwa kwa sababu ya makosa yake? Lakini kama mkiteswa kwa sababu ya kutenda mema, nanyi mkastahimili, hili ni jambo la kusifiwa mbele za Mungu. Ninyi mliitwa kwa ajili ya haya, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake. “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.” Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tufe kwa mambo ya dhambi, bali tupate kuishi katika haki. Kwa kupigwa kwake, ninyi mmeponywa.