Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 15:12-34

1 Wakorintho 15:12-34 BHN

Sasa, maadamu inahubiriwa kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, baadhi yenu wanawezaje kusema kwamba hakuna ufufuo wa wafu? Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka; na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yenu haina maana. Zaidi ya hayo sisi tungekuwa mashahidi wa uongo mbele ya Mungu, maana tulisema kwamba Mungu alimfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumbe yeye hakumfufua – kama ni kweli kwamba wafu hawafufuliwi. Maana, ikiwa ni kweli kwamba wafu hawafufuki, basi naye Kristo hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuliwa, basi, imani yenu ni ya bure; mngali bado katika dhambi zenu. Zaidi ya hayo, wale wote waliokufa wakiwa wameungana na Kristo wamepotea kabisa. Kama matumaini yetu katika Kristo yanahusu tu maisha haya ya sasa, basi, sisi ni watu wa kusikitikiwa zaidi kuliko wengine wote duniani. Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, wa kwanza wa wale waliolala katika kifo. Maana kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo hivyo nako kufufuka kutoka kwa wafu kumesababishwa na mtu mmoja. Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo. Lakini kila mmoja kwa mpango wake: Kristo kwanza; halafu wale walio wake Kristo wakati Kristo atakapokuja. Baada ya hayo, mwisho utafika wakati ambapo Kristo atamkabidhi Mungu Baba ufalme, baada ya kufutilia mbali kila tawala na mamlaka na nguvu. Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda maadui zake wote na kuwaweka chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo. Maana, Maandiko yasema: “Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini, Maandiko yanaposema: “Vitu vyote vimewekwa chini ya miguu yake avitawale” ni dhahiri kwamba Mungu haingii katika kundi hilo la vitu, maana yeye ndiye anayeviweka vitu hivyo chini ya Kristo. Lakini vitu vyote vitakapowekwa chini ya utawala wa Kristo, ndipo naye Mwana atakapojiweka chini ya Mungu, aliyeweka vyote chini ya utawala wake; ili Mungu atawale juu ya vyote. Kama hakuna ufufuo, je watu wale wanaobatizwa kwa ajili ya wafu wanatumainia kupata nini? Kama wafu hawafufuliwi, ya nini kubatizwa kwa ajili yao? Na sisi, ya nini kujitia hatarini kila saa? Ndugu, mimi nakikabili kifo kila siku! Fahari niliyo nayo juu yenu katika kuungana na Kristo Yesu Bwana wetu inanifanya nitangaze jambo hili. Kama kusudi langu lingalikuwa la kibinadamu tu, kule kupigana kwangu na wanyama wakali hapa Efeso kungalinifaa kitu gani? Kama wafu hawafufuki, basi, “Tule na tunywe, maana kesho tutakufa.” Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema. Amkeni! Anzeni kuishi vema, na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hawamjui Mungu kabisa. Hii nawaambieni, ni aibu kubwa kwenu!