Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 15:12-34

1 Wakorintho 15:12-34 NEN

Basi kama tumehubiri ya kwamba Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu, mbona baadhi yenu mnasema hakuna ufufuo wa wafu? Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Kristo hakufufuliwa. Tena ikiwa Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu, kuhubiri kwetu kumekuwa ni bure na imani yenu ni batili. Zaidi ya hayo, twaonekana kuwa mashahidi wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumeshuhudia kumhusu Mungu kwamba alimfufua Kristo kutoka kwa wafu, lakini hilo haliwezi kuwa kweli kama wafu hawafufuliwi. Kwa kuwa kama wafu hawafufuliwi, basi hata Kristo hajafufuka. Tena kama Kristo hajafufuliwa, imani yenu ni batili; nanyi bado mko katika dhambi zenu. Hivyo basi, wote waliolala katika Kristo wamepotea. Ikiwa tumaini letu ndani ya Kristo ni kwa ajili ya maisha haya tu, sisi tunastahili kuhurumiwa kuliko watu wote. Lakini kweli Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, tunda la kwanza la wale wote waliolala. Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kwa njia ya mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kwa njia ya mtu mmoja. Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Kristo wote watafanywa hai. Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Kristo, tunda la kwanza kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja. Ndipo mwisho utafika, wakati atakapomkabidhi Mungu Baba ufalme, akiisha angamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu. Kwa maana lazima Kristo atawale mpaka awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti. Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Kristo hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa. Atakapokuwa amekwisha kuyafanya haya, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote. Basi kama hakuna ufufuo, watafanyaje wale wabatizwao kwa ajili ya wafu? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, mbona watu wanabatizwa kwa ajili yao? Nasi kwa upande wetu kwa nini tunajihatarisha kila saa? Kama majivuno yangu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu ni kweli, ndugu zangu, ninakufa kila siku. Kama kwa sababu za kibinadamu tu nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, ningekuwa nimepata faida gani? Kama wafu hawafufuliwi, “Tuleni na kunywa, kwa kuwa kesho tutakufa.” Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.” Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, wala msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.