Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 15:12-34

1 Wakorintho 15:12-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Sasa, maadamu inahubiriwa kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, baadhi yenu wanawezaje kusema kwamba hakuna ufufuo wa wafu? Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka; na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yenu haina maana. Zaidi ya hayo sisi tungekuwa mashahidi wa uongo mbele ya Mungu, maana tulisema kwamba Mungu alimfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumbe yeye hakumfufua – kama ni kweli kwamba wafu hawafufuliwi. Maana, ikiwa ni kweli kwamba wafu hawafufuki, basi naye Kristo hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuliwa, basi, imani yenu ni ya bure; mngali bado katika dhambi zenu. Zaidi ya hayo, wale wote waliokufa wakiwa wameungana na Kristo wamepotea kabisa. Kama matumaini yetu katika Kristo yanahusu tu maisha haya ya sasa, basi, sisi ni watu wa kusikitikiwa zaidi kuliko wengine wote duniani. Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, wa kwanza wa wale waliolala katika kifo. Maana kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo hivyo nako kufufuka kutoka kwa wafu kumesababishwa na mtu mmoja. Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo. Lakini kila mmoja kwa mpango wake: Kristo kwanza; halafu wale walio wake Kristo wakati Kristo atakapokuja. Baada ya hayo, mwisho utafika wakati ambapo Kristo atamkabidhi Mungu Baba ufalme, baada ya kufutilia mbali kila tawala na mamlaka na nguvu. Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda maadui zake wote na kuwaweka chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo. Maana, Maandiko yasema: “Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini, Maandiko yanaposema: “Vitu vyote vimewekwa chini ya miguu yake avitawale” ni dhahiri kwamba Mungu haingii katika kundi hilo la vitu, maana yeye ndiye anayeviweka vitu hivyo chini ya Kristo. Lakini vitu vyote vitakapowekwa chini ya utawala wa Kristo, ndipo naye Mwana atakapojiweka chini ya Mungu, aliyeweka vyote chini ya utawala wake; ili Mungu atawale juu ya vyote. Kama hakuna ufufuo, je watu wale wanaobatizwa kwa ajili ya wafu wanatumainia kupata nini? Kama wafu hawafufuliwi, ya nini kubatizwa kwa ajili yao? Na sisi, ya nini kujitia hatarini kila saa? Ndugu, mimi nakikabili kifo kila siku! Fahari niliyo nayo juu yenu katika kuungana na Kristo Yesu Bwana wetu inanifanya nitangaze jambo hili. Kama kusudi langu lingalikuwa la kibinadamu tu, kule kupigana kwangu na wanyama wakali hapa Efeso kungalinifaa kitu gani? Kama wafu hawafufuki, basi, “Tule na tunywe, maana kesho tutakufa.” Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema. Amkeni! Anzeni kuishi vema, na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hawamjui Mungu kabisa. Hii nawaambieni, ni aibu kubwa kwenu!

1 Wakorintho 15:12-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu? Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure. Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama tumemtumaini Kristo katika maisha haya tu, sisi tu watu wa kusikitikiwa ziadi kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja. Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu. Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke adui zake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti. Kwa kuwa, Alivitiisha vitu vyote chini ya miguu yake. Lakini atakaposema, Vyote vimetiishwa, ni dhahiri ya kuwa yeye aliyemtiishia vitu vyote hayumo. Basi, vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake, ndipo Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba Mungu awe yote katika wote. Au je! Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu watafanyaje? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao? Na sisi, kwa nini tumo hatarini kila saa? Naam, ndugu, kwa huku kujisifu kwangu niliko nako juu yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu, ninakufa kila siku. Ikiwa, kwa jinsi ya kibinadamu, nilipigana na hayawani wakali kule Efeso, nina faida gani? Wasipofufuliwa wafu, na tule, na tunywe, maana kesho tutakufa. Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.

1 Wakorintho 15:12-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu? Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure. Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja. Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu. Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti. Kwa kuwa, Alivitiisha vitu vyote chini ya miguu yake. Lakini atakaposema, Vyote vimetiishwa, ni dhahiri ya kuwa yeye aliyemtiishia vitu vyote hayumo. Basi, vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake, ndipo Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba Mungu awe yote katika wote. Au je! Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu watafanyaje? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao? Na sisi, kwa nini tumo hatarini kila saa? Naam, ndugu, kwa huku kujisifu kwangu niliko nako juu yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu, ninakufa kila siku. Ikiwa, kwa jinsi ya kibinadamu, nalipigana na hayawani wakali kule Efeso, nina faida gani? Wasipofufuliwa wafu, na tule, na tunywe, maana kesho tutakufa. Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.

1 Wakorintho 15:12-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi kama tumehubiri ya kwamba Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu, mbona baadhi yenu mnasema hakuna ufufuo wa wafu? Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Kristo hakufufuliwa. Tena ikiwa Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu, kuhubiri kwetu kumekuwa ni bure na imani yenu ni batili. Zaidi ya hayo, twaonekana kuwa mashahidi wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumeshuhudia kumhusu Mungu kwamba alimfufua Kristo kutoka kwa wafu, lakini hilo haliwezi kuwa kweli kama wafu hawafufuliwi. Kwa kuwa kama wafu hawafufuliwi, basi hata Kristo hajafufuka. Tena kama Kristo hajafufuliwa, imani yenu ni batili; nanyi bado mko katika dhambi zenu. Hivyo basi, wote waliolala katika Kristo wamepotea. Ikiwa tumaini letu ndani ya Kristo ni kwa ajili ya maisha haya tu, sisi tunastahili kuhurumiwa kuliko watu wote. Lakini kweli Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, tunda la kwanza la wale wote waliolala. Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kwa njia ya mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kwa njia ya mtu mmoja. Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Kristo wote watafanywa hai. Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Kristo, tunda la kwanza kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja. Ndipo mwisho utafika, wakati atakapomkabidhi Mungu Baba ufalme, akiisha angamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu. Kwa maana lazima Kristo atawale mpaka awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti. Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Kristo hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa. Atakapokuwa amekwisha kuyafanya haya, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote. Basi kama hakuna ufufuo, watafanyaje wale wabatizwao kwa ajili ya wafu? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, mbona watu wanabatizwa kwa ajili yao? Nasi kwa upande wetu kwa nini tunajihatarisha kila saa? Kama majivuno yangu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu ni kweli, ndugu zangu, ninakufa kila siku. Kama kwa sababu za kibinadamu tu nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, ningekuwa nimepata faida gani? Kama wafu hawafufuliwi, “Tuleni na kunywa, kwa kuwa kesho tutakufa.” Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.” Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, wala msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.