1 Mambo ya Nyakati 16:7-36
1 Mambo ya Nyakati 16:7-36 BHN
Basi, hiyo ikawa siku ambayo kwa mara ya kwanza, Daudi alimpa Asafu na ndugu zake Walawi wajibu wa kumwimbia Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani. Mpeni shukrani Mwenyezi-Mungu, tangazeni ukuu wake, yajulisheni mataifa mambo aliyoyatenda! Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa; simulieni matendo yake ya ajabu! Jisifieni jina lake takatifu; wenye kumcha Mwenyezi-Mungu na wafurahi. Mwendeeni Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu; mwendeeni Mwenyezi-Mungu daima. Kumbukeni matendo ya ajabu aliyotenda, maajabu yake na hukumu alizotoa, enyi wazawa wa Abrahamu, mtumishi wake, enyi wazawa wa Yakobo, wateule wake. Yeye Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu; hukumu zake zina nguvu duniani kote. Yeye hulishika agano lake milele, hutimiza ahadi zake kwa vizazi elfu. Hushika agano alilofanya na Abrahamu, na ahadi aliyomwapia Isaka. Alimthibitishia Yakobo ahadi yake, akamhakikishia agano hilo la milele. Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani, nayo itakuwa mali yenu wenyewe.” Idadi yenu ilikuwa ndogo, mlikuwa wachache na wageni katika nchi ya Kanaani, mkitangatanga toka taifa hadi taifa, kutoka nchi moja hadi nchi nyingine, Mungu hakumruhusu mtu yeyote awadhulumu; kwa ajili yao aliwaonya wafalme: “Msiwaguse wateule wangu; msiwadhuru manabii wangu!” Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote. Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu. Yatangazieni mataifa utukufu wake, waambieni watu wote matendo yake ya ajabu. Maana Mwenyezi-Mungu ni mkuu, anasifika sana anastahili kuheshimiwa kuliko miungu yote. Miungu yote ya mataifa mengine si kitu; lakini Mwenyezi-Mungu aliziumba mbingu. Utukufu na fahari vyamzunguka, nguvu na furaha vyajaza hekalu lake. Mpeni Mwenyezi-Mungu, heshima enyi jamii zote za watu, naam, kirini utukufu na nguvu yake. Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima ya utukufu wa jina lake; leteni tambiko na kuingia nyumbani mwake. Mwabuduni Mwenyezi-Mungu patakatifuni pake. Ee dunia yote; tetemeka mbele yake! Ameuweka ulimwengu imara, hautatikisika. Furahini enyi mbingu na dunia! Yaambieni mataifa, “Mwenyezi-Mungu anatawala!” Bahari na ivume, pamoja na vyote vilivyomo! Furahini enyi mashamba na vyote vilivyomo! Ndipo miti yote msituni itaimba kwa furaha mbele ya Mwenyezi-Mungu anayekuja naam, anayekuja kuihukumu dunia. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele! Mwambieni Mwenyezi-Mungu: Utuokoe, ee Mungu wa wokovu wetu, utukusanye pamoja na kutuokoa kutoka kwa mataifa, tupate kulisifu jina lako takatifu, kuona fahari juu ya sifa zako. Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele! Kisha watu wote wakasema, “Amina!” Pia wakamsifu Mwenyezi-Mungu.