Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Nyakati 16:7-36

1 Nyakati 16:7-36 NEN

Siku ile, kitu cha kwanza Daudi alichofanya ni kumkabidhi Asafu na wenzake zaburi hii ya shukrani kwa BWANA: Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda. Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa; waambieni matendo yake yote ya ajabu. Lishangilieni jina lake takatifu; mioyo ya wale wamtafutao BWANA na ifurahi. Mtafuteni BWANA na nguvu zake; utafuteni uso wake siku zote. Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya, miujiza yake na hukumu alizozitamka, enyi wazao wa Israeli mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye ndiye BWANA Mungu wetu; hukumu zake zimo duniani pote. Hulikumbuka agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu, agano alilolifanya na Abrahamu, kiapo alichomwapia Isaki. Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri, kwa Israeli liwe agano la milele: “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani kuwa sehemu utakayoirithi.” Walipokuwa wachache kwa idadi, wachache sana na wageni ndani yake, walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine, kutoka ufalme mmoja hadi mwingine. Hakuruhusu mtu yeyote awaonee; kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema: “Msiwaguse niliowatia mafuta; msiwadhuru manabii wangu.” Mwimbieni BWANA dunia yote; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku. Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa, matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote. Kwa kuwa BWANA ni mkuu, mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote. Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini BWANA aliziumba mbingu. Fahari na enzi viko mbele yake; nguvu na utukufu vimo patakatifu pake. Mpeni BWANA, enyi jamaa za mataifa, mpeni BWANA utukufu na nguvu, mpeni BWANA utukufu unaostahili jina lake. Leteni sadaka na mje katika nyua zake; mwabuduni BWANA katika uzuri wa utakatifu wake. Dunia yote na itetemeke mbele zake! Ulimwengu ameuweka imara; hauwezi kusogezwa. Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; semeni katikati ya mataifa, “BWANA anatawala!” Bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake; mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo ndani yake. Kisha miti ya msituni itaimba, itaimba kwa furaha mbele za BWANA, kwa maana anakuja kuihukumu dunia. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele. Mlilieni, “Ee Mungu Mwokozi wetu, tuokoe. Tukusanye tena na utukomboe kutoka kwa mataifa, ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu, na kushangilia katika sifa zako.” Atukuzwe BWANA, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Nao watu wote wakasema, “Amen,” na “Msifuni BWANA.”