Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 15:1-24

1 Mambo ya Nyakati 15:1-24 BHN

Daudi alijijengea nyumba katika mji wa Daudi. Tena akalitengenezea sanduku la Mungu mahali, akalipigia hema. Kisha akasema, “Hakuna mtu mwingine yeyote atakayelibeba sanduku la Mungu isipokuwa Walawi, maana Mwenyezi-Mungu aliwachagua wao kulibeba na kumtumikia milele.” Basi, akawakusanya Waisraeli wote waje Yerusalemu, ili kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu mahali alipolitayarishia. Halafu Daudi akawaita wazawa wa Aroni na Walawi: Kutoka katika ukoo wa Kohathi, wakaja Urieli, pamoja na ndugu zake120 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo wa Merari wakaja Asaya pamoja na ndugu zake 220 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo wa Gershomu, wakaja Yoeli pamoja na ndugu zake 130 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo ya Elisafani, wakaja Shemaya pamoja na ndugu zake 200 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo wa Hebroni, wakaja Elieli pamoja na ndugu zake 80 chini ya usimamizi wake; na kutoka katika ukoo wa Uzieli, wakaja Aminadabu pamoja na ndugu zake 112 chini ya usimamizi wake. Daudi akawaita makuhani wawili: Sadoki na Abiathari, na Walawi sita: Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu; akawaambia, “Nyinyi ni viongozi wa koo za Walawi. Jitakaseni pamoja na ndugu zenu, ili mkalilete sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hadi mahali ambapo nimelitayarishia. Kwa sababu hamkulibeba safari ya kwanza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alituadhibu kwani hatukulitunza kama alivyoagiza.” Basi, makuhani na Walawi wakajitakasa ili wapate kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Walawi wakalibeba mabegani mwao wakitumia mipiko yake kama Mose alivyoamuru, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu. Daudi pia aliwaamuru wakuu wa Walawi wachague baadhi ya ndugu zao wawe wakiimba na kupiga ala za muziki: Vinanda, vinubi na matoazi kwa nguvu, ili kutoa sauti za furaha. Hivyo wakachagua watu wafuatao katika koo za waimbaji: Hemani mwana wa Yoeli, Asafu nduguye aliyekuwa mwana wa Berekia na wana wa Merari, ndugu zao, na Ethani mwana wa Kushaya. Kisha wakawachagua Walawi wafuatao wawe wasaidizi wao kwa kushika nafasi ya pili: Zekaria, Yaasieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Benaya, Maaseya, Matithia, Elifelehu na Mikneya na walinzi wa lango: Obed-edomu na Yeieli. Hemani, Asafu na Etani wakachaguliwa kupiga matoazi ya Shaba. Zekaria, Azieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Maaseya na Benaya, walikuwa wapiga vinubi vya sauti ya Alamothi. Lakini Matithia, Elifelehu, Mikneya, Obed-edomu, Yeieli na Azazia waliongoza wakiwa na vinubi vya sauti ya Sheminithi. Naye Kenania kwa sababu ya ujuzi wa muziki aliokuwa nao, aliwekwa kuwa kiongozi wa wote. Berekia na Elkana walikuwa walinzi wa sanduku la agano. Shebania, Yoshafati, Nethaneli, Amasai, Zekaria, Benaya na Eliezeri, waliokuwa makuhani, waliwekwa kupiga tarumbeta mbele ya sanduku la Mungu. Obed-edomu na Yehiya waliwekwa pia kuwa walinzi wa sanduku.