Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 15:1-24

1 Mambo ya Nyakati 15:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Daudi alijijengea nyumba katika mji wa Daudi. Tena akalitengenezea sanduku la Mungu mahali, akalipigia hema. Kisha akasema, “Hakuna mtu mwingine yeyote atakayelibeba sanduku la Mungu isipokuwa Walawi, maana Mwenyezi-Mungu aliwachagua wao kulibeba na kumtumikia milele.” Basi, akawakusanya Waisraeli wote waje Yerusalemu, ili kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu mahali alipolitayarishia. Halafu Daudi akawaita wazawa wa Aroni na Walawi: Kutoka katika ukoo wa Kohathi, wakaja Urieli, pamoja na ndugu zake120 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo wa Merari wakaja Asaya pamoja na ndugu zake 220 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo wa Gershomu, wakaja Yoeli pamoja na ndugu zake 130 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo ya Elisafani, wakaja Shemaya pamoja na ndugu zake 200 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo wa Hebroni, wakaja Elieli pamoja na ndugu zake 80 chini ya usimamizi wake; na kutoka katika ukoo wa Uzieli, wakaja Aminadabu pamoja na ndugu zake 112 chini ya usimamizi wake. Daudi akawaita makuhani wawili: Sadoki na Abiathari, na Walawi sita: Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu; akawaambia, “Nyinyi ni viongozi wa koo za Walawi. Jitakaseni pamoja na ndugu zenu, ili mkalilete sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hadi mahali ambapo nimelitayarishia. Kwa sababu hamkulibeba safari ya kwanza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alituadhibu kwani hatukulitunza kama alivyoagiza.” Basi, makuhani na Walawi wakajitakasa ili wapate kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Walawi wakalibeba mabegani mwao wakitumia mipiko yake kama Mose alivyoamuru, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu. Daudi pia aliwaamuru wakuu wa Walawi wachague baadhi ya ndugu zao wawe wakiimba na kupiga ala za muziki: Vinanda, vinubi na matoazi kwa nguvu, ili kutoa sauti za furaha. Hivyo wakachagua watu wafuatao katika koo za waimbaji: Hemani mwana wa Yoeli, Asafu nduguye aliyekuwa mwana wa Berekia na wana wa Merari, ndugu zao, na Ethani mwana wa Kushaya. Kisha wakawachagua Walawi wafuatao wawe wasaidizi wao kwa kushika nafasi ya pili: Zekaria, Yaasieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Benaya, Maaseya, Matithia, Elifelehu na Mikneya na walinzi wa lango: Obed-edomu na Yeieli. Hemani, Asafu na Etani wakachaguliwa kupiga matoazi ya Shaba. Zekaria, Azieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Maaseya na Benaya, walikuwa wapiga vinubi vya sauti ya Alamothi. Lakini Matithia, Elifelehu, Mikneya, Obed-edomu, Yeieli na Azazia waliongoza wakiwa na vinubi vya sauti ya Sheminithi. Naye Kenania kwa sababu ya ujuzi wa muziki aliokuwa nao, aliwekwa kuwa kiongozi wa wote. Berekia na Elkana walikuwa walinzi wa sanduku la agano. Shebania, Yoshafati, Nethaneli, Amasai, Zekaria, Benaya na Eliezeri, waliokuwa makuhani, waliwekwa kupiga tarumbeta mbele ya sanduku la Mungu. Obed-edomu na Yehiya waliwekwa pia kuwa walinzi wa sanduku.

1 Mambo ya Nyakati 15:1-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya Daudi kujijengea nyumba zake katika Mji wa Daudi, akatengeneza sehemu kwa ajili ya Sanduku la Mungu, kisha akasimamisha hema kwa ajili yake. Kisha Daudi akasema, “Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kulibeba Sanduku la Mungu isipokuwa Walawi peke yao, kwa sababu BWANA aliwachagua kulibeba Sanduku la BWANA na kuhudumu mbele zake milele.” Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu ili kulipandisha Sanduku la BWANA na kulileta hadi kwenye sehemu aliyokuwa ametengeneza kwa ajili yake. Kisha Daudi akawakusanya pamoja wazao wa Aroni na Walawi: Kutoka wazao wa Kohathi, Urieli kiongozi na ndugu zake 120, Kutoka wazao wa Merari, Asaya kiongozi na ndugu zake 220. Kutoka wazao wa Gershoni, Yoeli kiongozi na ndugu zake 130. Kutoka wazao wa Elisafani, Shemaya kiongozi na ndugu zake 200. Kutoka wazao wa Hebroni, Elieli kiongozi na ndugu zake 80. Kutoka wazao wa Uzieli, Aminadabu kiongozi na ndugu zake 112. Kisha Daudi akawaita makuhani Sadoki na Abiathari, pamoja na Walawi Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu. Akawaambia, “Ninyi ndio viongozi wa jamaa za Walawi. Ninyi pamoja na Walawi wenzenu inawapasa mjitakase na kulipandisha Sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli hadi mahali ambapo nimetengeneza kwa ajili yake. Ilikuwa ni kwa sababu hii, ninyi Walawi, hamkulipandisha Sanduku la BWANA mara ya kwanza, hata ikasababisha BWANA Mungu wetu kuwaka hasira dhidi yetu. Hatukumuuliza jinsi ya kufanya ili tupate kulileta jinsi alivyoagiza.” Kwa hiyo makuhani pamoja na Walawi wakajitakasa ili kulipandisha Sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli. Nao Walawi wakalichukua Sanduku la Mungu mabegani mwao wakitumia mipiko, kama vile Mose alivyoamuru sawasawa na neno la BWANA. Daudi akawaambia viongozi wa Walawi kuwaweka ndugu zao waimbaji ili waimbe nyimbo za shangwe, wakiwa na vyombo vya uimbaji: zeze, vinubi na matoazi. Basi Walawi wakawaweka Hemani mwana wa Yoeli; kutoka miongoni mwa ndugu zake, Asafu mwana wa Berekia; kutoka miongoni mwa ndugu zao Wamerari, Ethani mwana wa Kushaiya; hawa ndio waliochaguliwa kuwa wasaidizi wao: Zekaria, Yaazieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Benaya, Maaseya, Matithia, Elifelehu, Mikneya, pamoja na mabawabu Obed-Edomu na Yehieli. Waimbaji Hemani, Asafu na Ethani walichaguliwa kupiga matoazi ya shaba; Zekaria, Azieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Maaseya na Benaya walikuwa wapiga zeze kufuatana na sauti ya alamothi, na Matithia, Elifelehu, Mikneya, Obed-Edomu, Yehieli na Azazia walikuwa wapiga vinubi, wakiongozwa kwa kufuata sauti ya sheminithi. Kenania kiongozi wa Walawi alikuwa msimamizi wa uimbaji; huu ndio uliokuwa wajibu wake kwa sababu alikuwa stadi katika hilo. Berekia na Elikana walikuwa mabawabu kwa ajili ya Sanduku. Shebania, Yoshafati, Nethaneli, Amasai, Zekaria, Benaya na Eliezeri, makuhani, walikuwa wapiga tarumbeta mbele ya Sanduku la Mungu. Obed-Edomu na Yehiya waliwekwa pia kuwa mabawabu wa Sanduku.

1 Mambo ya Nyakati 15:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Daudi akajijengea nyumba katika mji wa Daudi; akatayarisha mahali kwa ajili ya sanduku la Mungu, akalipigia hema. Ndipo Daudi akasema, Haimpasi mtu awaye yote kulichukua sanduku la Mungu, isipokuwa Walawi peke yao; kwa kuwa hao ndio aliowachagua BWANA, ili walichukue sanduku la Mungu, na kumtumikia daima. Basi Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu, ili kulipandisha sanduku la BWANA, mpaka mahali pake alipoliwekea tayari. Daudi akawakutanisha wana wa Haruni, na Walawi; wa wana wa Kohathi; Urieli mkuu wao, na nduguze mia moja na ishirini; wa wana wa Merari; Asaya mkuu wao, na nduguze mia mbili na ishirini; wa wana wa Gershoni; Yoeli mkuu wao, na nduguze mia moja na thelathini; wa wana wa Elsafani; Shemaya mkuu wao, na nduguze mia mbili; wa wana wa Hebroni; Elieli mkuu wao, na nduguze themanini; wa wana wa Uzieli; Aminadabu mkuu wao, na nduguze mia moja kumi na wawili. Tena, Daudi akawaita Sadoki na Abiathari makuhani, na hao Walawi, Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli, na Aminadabu, akawaambia, Ninyi ni vichwa vya koo za baba za Walawi; jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipolitayarishia. Kwa kuwa ninyi hamkulichukua safari ya kwanza, BWANA, Mungu wetu, alitufurikia, kwa maana hatukumtafuta kulingana na sheria. Basi makuhani na Walawi wakajitakasa, ili wapate kulipandisha sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli. Na wana wa Walawi wakalichukua sanduku la Mungu mabegani mwao kwa miti yake, kama vile Musa alivyoamuru, kulingana na neno la BWANA. Kisha Daudi akamwambia mkuu wa Walawi, kwamba awaagize ndugu zao waimbaji, pamoja na vyombo vyao vya kupigia ngoma, vinanda, na vinubi, na matoazi, wavipige na kupaza sauti kwa furaha. Basi Walawi wakamwagiza Hemani mwana wa Yoeli; na wa nduguze, Asafu mwana wa Berekia; na wa wana wa Merari ndugu zao, Ethani mwana wa Kishi; na pamoja nao ndugu zao kwa cheo cha pili, Zekaria, na Yaasieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu; na Benaya, na Maaseya, na Matithia, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, mabawabu. Hivyo hao waimbaji, Hemani, Asafu, na Ethani, wakaagizwa kupiga matoazi yao ya shaba kwa sauti kuu; na Zekaria, na Yaasieli na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu, na Maaseya, na Benaya, wenye vinanda vya sauti ya Alamothi; na Metithia, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, na Azazia, wenye vinubi vya sauti ya Sheminithi, waongoze. Na Kenania, mkuu wa Walawi katika uimbaji, asimamie uimbaji, kwa sababu alikuwa stadi. Na Berekia na Elkana walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku. Na Shebania, na Yoshafati, na Nethaneli, na Amasai, na Zekaria, na Benaya, na Eliezeri, makuhani, wakapiga baragumu mbele ya sanduku la Mungu; na Obed-edomu na Yehia walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku.

1 Mambo ya Nyakati 15:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Daudi akajifanyia nyumba katika mji wa Daudi; akapaweka tayari mahali kwa ajili ya sanduku la Mungu, akalipigia hema. Ndipo Daudi akasema, Haimpasi mtu awaye yote kulichukua sanduku la Mungu, isipokuwa Walawi peke yao; kwa kuwa hao ndio aliowachagua BWANA, ili walichukue sanduku la Mungu, na kumtumikia daima. Basi Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu, ili kulipandisha sanduku la BWANA, mpaka mahali pake alipoliwekea tayari. Daudi akawakutanisha wana wa Haruni, na Walawi; wa wana wa Kohathi; Urieli mkuu wao, na nduguze mia na ishirini; wa wana wa Merari; Asaya mkuu wao, na nduguze mia mbili na ishirini; wa wana wa Gershoni; Yoeli mkuu wao, na nduguze mia na thelathini; wa wana wa Elsafani; Shemaya mkuu wao, na nduguze mia mbili; wa wana wa Hebroni; Elieli mkuu wao, na nduguze themanini; wa wana wa Uzieli; Aminadabu mkuu wao, na nduguze mia na kumi na wawili. Tena, Daudi akawaita Sadoki na Abiathari makuhani, na hao Walawi, Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli, na Aminadabu, akawaambia, Ninyi ni vichwa vya mbari za baba za Walawi; jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipoliwekea tayari. Kwani kwa sababu ninyi hamkulichukua safari ya kwanza, BWANA, Mungu wetu, alitufurikia, kwa maana hatukumtafuta sawasawa na sheria. Basi makuhani na Walawi wakajitakasa, ili wapate kulipandisha sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli. Na wana wa Walawi wakalichukua sanduku la Mungu mabegani mwao kwa miti yake, kama vile Musa alivyoamuru, sawasawa na neno la BWANA. Kisha Daudi akamwambia mkuu wa Walawi, kwamba awaagize ndugu zao waimbaji, pamoja na vyombo vyao vya kupigia ngoma, vinanda, na vinubi, na matoazi, wavipige na kupaza sauti kwa furaha. Basi Walawi wakamwagiza Hemani mwana wa Yoeli; na wa nduguze, Asafu mwana wa Berekia; na wa wana wa Merari ndugu zao, Ethani mwana wa Kishi; na pamoja nao ndugu zao kwa cheo cha pili, Zekaria, na Yaasieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu; na Benaya, na Maaseya, na Matithia, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, mabawabu. Hivyo hao waimbaji, Hemani, Asafu, na Ethani, wakaagizwa kupiga matoazi yao ya shaba kwa sauti kuu; na Zekaria, na Yaasieli na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu, na Maaseya, na Benaya, wenye vinanda vya sauti ya Alamothi; na Matithiya, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, na Azazia, wenye vinubi vya sauti ya Sheminithi, waongoze. Na Kenania, mkuu wa Walawi, alikuwa juu ya uchukuzi; yeye aliusimamia uchukuzi, kwa sababu alikuwa mstadi. Na Berekia na Elkana walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku. Na Shebania, na Yoshafati, na Nethaneli, na Amasai, na Zekaria, na Benaya, na Eliezeri, makuhani, wakapiga baragumu mbele ya sanduku la Mungu; na Obed-edomu na Yehia walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku.