Mwanzo 34
34
Dina na Washekemu
1Basi Dina, binti Yakobo aliyezaliwa na Lea, akaenda kuwatembelea wanawake wa nchi ile. 2Ikawa Shekemu mwana wa Hamori Mhivi, mtawala wa eneo lile, alipomwona, akamchukua na kumnajisi. 3Moyo wake ukavutwa sana kwa Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana na akazungumza naye kwa kumbembeleza. 4Shekemu akamwambia Hamori, baba yake, “Nipatie msichana huyu awe mke wangu.”
5Yakobo aliposikia kwamba binti yake Dina amenajisiwa, wanawe walikuwa mashambani wakichunga mifugo yake. Kwa hiyo akalinyamazia jambo hilo hadi waliporudi nyumbani.
6Kisha Hamori baba yake Shekemu akaenda kuzungumza na Yakobo. 7Basi wana wa Yakobo wakarudi kutoka mashambani mara tu waliposikia kilichotukia. Walijawa na huzuni na ghadhabu, kwa sababu Shekemu alikuwa amefanya jambo la aibu katika Israeli kwa kukutana kimwili na binti Yakobo, jambo ambalo halikupasa kutendwa.
8Lakini Hamori akawaambia, “Moyo wa mwanangu Shekemu umeelekea kwa binti yenu. Tafadhali mpeni awe mke wake. 9Oaneni na sisi; tupeni binti zenu, nanyi mchukue binti zetu. 10Mwaweza kuishi nasi, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, mfanye biashara humu na mjipatie mali.”
11Kisha Shekemu akamwambia baba yake Dina pamoja na ndugu zake, “Naomba nipate kibali machoni penu, nami nitawapa chochote mtakachosema. 12Niambieni kiasi cha mahari na zawadi nitakayoileta, hata iwe kubwa kiasi gani, nami nitawalipa chochote mtakachodai. Nipeni tu huyu msichana awe mke wangu.”
13Kwa sababu dada yao Dina alikuwa amenajisiwa, wana wa Yakobo wakajibu kwa udanganyifu walipozungumza na Shekemu pamoja na Hamori, baba yake. 14Wakawaambia, “Hatuwezi kufanya jambo kama hili. Hatuwezi kumtoa dada yetu kwa mtu ambaye hajatahiriwa. Hiyo itakuwa aibu kwetu. 15Tutakuruhusu kwa sharti moja tu, kwamba mtakuwa kama sisi kwa kuwatahiri wanaume wenu wote. 16Kisha tutawapa binti zetu na sisi tutawachukua binti zenu. Tutaishi kwenu na tutakuwa watu wamoja nanyi. 17Lakini mkikataa kutahiriwa, tutamchukua dada yetu na kuondoka.”
18Pendekezo lao likakubalika kwa Hamori na Shekemu mwanawe. 19Kijana huyo, aliyekuwa ameheshimiwa kati ya wote walioishi nyumbani mwa baba yake, hakupoteza muda kufanya waliyoyasema, kwa sababu alikuwa amependezwa sana na binti Yakobo. 20Kwa hiyo Hamori na Shekemu mwanawe walienda kwenye lango la mji kuzungumza na wanaume wa mji wao. 21Wakasema, “Hawa wanaume ni rafiki zetu. Tuwaruhusu waishi katika nchi yetu na kufanya biashara ndani yake; nchi ina nafasi tele kwa ajili yao. Tunaweza kuoa binti zao, nao wanaweza kuoa binti zetu. 22Lakini wanaume hawa watakubali kuishi nasi kama watu wamoja nao kwa sharti kwamba wanaume wetu watahiriwe, kama wao. 23Je, si mifugo yao, mali yao na wanyama wao wengine wote watakuwa wetu? Basi tukubali sharti lao, nao wataishi miongoni mwetu.”
24Wanaume wote waliotoka nje ya lango la mji walikubaliana na Hamori na Shekemu mwanawe, na kila mwanaume katika mji ule akatahiriwa.
25Baada ya siku tatu, wakati wote wakiwa wangali katika maumivu, wana wawili wa Yakobo, yaani Simeoni na Lawi, ndugu zake Dina, wakachukua panga zao na kuvamia mji ambao haukutazamia vita, wakaua kila mwanaume. 26Wakawaua Hamori na Shekemu mwanawe kwa panga, kisha wakamchukua Dina kutoka nyumba ya Shekemu na kuondoka. 27Wana hao wengine wa Yakobo wakaingia mji uliojaa maiti na kuteka nyara katika mji huo dada yao alikuwa amenajisiwa. 28Wakateka kondoo na mbuzi, ng’ombe, punda, na kila kitu kilichokuwa ndani ya mji ule na mashambani. 29Waliteka utajiri wao wote, pamoja na wanawake na watoto wao, wakapora kila kitu ndani ya nyumba zao.
30Kisha Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, “Mmenitaabisha kwa kunifanya ninuke kama uvundo kwa Wakanaani na Waperizi, watu wanaoishi nchi hii. Sisi ni wachache; wakiunganisha nguvu zao dhidi yangu na kunishambulia, mimi na nyumba yangu tutaangamizwa.”
31Lakini wakamjibu, “Je, ilikuwa vyema kumtendea dada yetu kama kahaba?”
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 34: ONMM
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ ONMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Biblica® Open Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.