Mwanzo 33
33
Yakobo akutana na Esau
1Yakobo akainua macho, akamwona Esau akija na watu wake mia nne. Kwa hiyo akawagawanya watoto kati ya Lea, Raheli na wale wajakazi wake wawili. 2Akawaweka wale wajakazi na watoto wao mbele, Lea na watoto wake wakafuata, nao Raheli na Yusufu wakaja nyuma. 3Yeye mwenyewe akatangulia mbele na kusujudu hadi chini mara saba alipomkaribia ndugu yake.
4Lakini Esau akamkimbilia Yakobo kumlaki na kumkumbatia, akamwangukia shingoni na kumbusu. Nao wakalia. 5Esau akainua macho, akawaona wale wanawake na watoto. Akauliza, “Hawa waliofuatana nawe ni nani?”
Yakobo akamjibu, “Ni watoto ambao Mungu amempa mtumishi wako kwa neema.”
6Kisha wale wajakazi na watoto wao wakakaribia na kusujudu. 7Kisha Lea na watoto wake wakaja na kusujudu. Mwisho wa wote wakaja Yusufu na Raheli, nao pia wakasujudu.
8Esau akauliza, “Makundi hayo yote niliyokutana nayo yana maana gani?”
Akasema, “Ni ili kupata kibali machoni pako, bwana wangu.”
9Lakini Esau akamwambia, “Ndugu yangu, tayari nina wingi wa mali. Ulivyo navyo viwe vyako mwenyewe.”
10Yakobo akasema, “La hasha! Tafadhali, kama nimepata kibali machoni pako, upokee zawadi hii kutoka kwangu. Kwa maana kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa kibali kikubwa. 11Tafadhali kubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea.
12Ndipo Esau akasema, “Tuendelee na safari; nitakusindikiza.”
13Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu, unajua kwamba watoto ni wachanga na kwamba ni lazima nitunze hawa ng’ombe na kondoo wanaonyonyesha. Wakipelekwa kwa haraka hata kama ni kwa siku moja tu, wanyama wote watakufa. 14Hivyo bwana wangu, mtangulie mtumishi wako, nami nije polepole kwa mwendo wa makundi yaliyo mbele yangu na mwendo wa watoto, hadi nifike kwa bwana wangu huko Seiri.”
15Esau akamwambia, “Basi kubali nikuachie baadhi ya watu wangu.”
Yakobo akauliza, “Lakini kwa nini ufanye hivyo? Niache tu nipate kibali machoni pa bwana wangu.”
16Hivyo siku hiyo Esau akashika njia, akarudi Seiri. 17Pamoja na hayo, Yakobo akaenda Sukothi#33:17 maana yake Vibanda. Akajijengea makazi na pia vibanda vya mifugo yake. Hii ndiyo sababu mahali pale panaitwa Sukothi.
18Baada ya Yakobo kutoka Padan-Aramu, alifika salama katika mji wa Shekemu huko Kanaani, na kuweka kambi yake karibu na mji huo. 19Akanunua kiwanja kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa bei ya vipande mia moja vya fedha, akapiga hema lake hapo. 20Akajenga madhabahu pale na kupaita El-Elohe-Israeli#33:20 maana yake Mungu, Mungu wa Israeli au Mwenye Nguvu ni Mungu wa Israeli.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 33: ONMM
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ ONMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Biblica® Open Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.